Habari

Operesheni yapata miili 14 mito ya Nairobi

May 25th, 2019 1 min read

Na MWANDISHI WETU

OPERESHENI kubwa ya kusafisha mito ya jiji la Nairobi imepata miili 14, baadhi ikiwa ya vijusi na watoto wadogo, serikali ya kaunti ilisema Ijumaa.

Ijumaa, wasafishaji walipata mwili wa kijana mwenye umri wa miaka minane aliyekuwa amenyongwa na kutupwa karibu na mto Nairobi, siku chache tu baada ya miili ya pacha wawili kupatikana ndani ya mfuko wa plastiki.

“Vijana wanaosafisha mto wa Nairobi walipata mwili mwingine wa mvulana aliyekuwa amenyongwa na kutupwa karibu na mto,” msemaji wa serikali ya Kaunti ya Nairobi, Elkana Jacob alisema.

“Hii inafikisha 14 miili ya watu wazima na watoto ambao wametolewa kutoka mito ya jiji la Nairobi tangu Gavana Mike Sonko azindue zoezi hili la usafi,” aliongeza Bw Jacob.

Jina la jiji la Nairobi linatokana na neno la Kimaasai lenye maana “pahali pa maji tulivu”.

Hata hivyo, mto mkuu na vijito vyake vimegeuzwa jaa la taka na viwanda na wakazi.

Hali ya kusikitisha

Viwanda vinaelekeza taka mitoni, huku msururu wa mitaa ya mabanda isiyo na mifumo ya kuondoa majitaka ikielekeza taka zote katika mto.

“Idadi ya miili iliyotolewa katika mito ya Nairobi inatia hofu. Tumepiga ripoti kwa polisi ili wafanye uchunguzi kubaini nani wanasababisha mauaji haya,” Gavana Sonko alisema katika taarifa jana.

Kando na miili minane ya watoto wachanga iliyopatikana Ijumaa pamoja na ule wa mvulana mdogo, miili mitano ya watu wazima pia ilipatikana mwaka huu kutoka kwa mto Nairobi na vijito vyake vya Ngong na Mathare wakati wa shughuli ya usafishaji.