Orengo awalaumu vigogo ODM kwa kumtoroka Raila

Orengo awalaumu vigogo ODM kwa kumtoroka Raila

Na VICTOR RABALLA

SENETA wa Siaya, James Orengo, amewakemea viongozi wa ODM kwa kumuacha kiongozi wa chama hicho Raila Odinga wakati anawahitaji zaidi.

Bw Orengo ameapa kutomuacha Bw Raila Odinga wakati kama huu ambapo waziri huyo mkuu wa zamani anajizatiti kuokoa mchakato wa mageuzi ya katiba kupitia mpango wa maridhiano (BBI).

Akiongea Jumamosi, mwanasiasa huyo ambaye ni Wakili Mkuu alisema kuwa inasikitisha kuwa baadhi ya viongozi huamua kumtelekeza Bw Odinga nyakati kama hizi anapokabiliwa na changomoto.

“Wakati kama huu, utawasikia wengine wanauliza Orengo yuko wapi ilhali wao ndio huwa mstari wa mbele kunishtumu wakidai ninamkosoa kiongozi wa chama chetu,” akasema alipohudhuria hafla ya mazishi katika Kaunti ya Siaya.

Bw Orengo ni miongoni mwa mawakili wenye uzoefu mkubwa walioteuliwa na Bw Odinga kumwakilisha katika kesi ya rufaa dhidi ya uamuzi wa Mahakama Kuu kuharamisha mchakato wa BBI. Wengine ni Mbunge wa Rarieda, Dkt Otiende Amollo, Bw Paul Mwangi, Bw Jackson Owele, Bw Ben Sihanya na Bw Arnold Oginga.

Bw Orengo, ambaye ni Kiongozi wa Wachache katika Seneti, alisema baadhi ya wanasiasa ndani ya ODM hawana uwezo wa kutetea chama hicho kama ilivyodhihirika hapo awali.

“Ni wachache tu waliojitokeza katika uwanja wa Uhuru Park mnamo Januari 30, 2018 tulipomwapisha Bw Odinga kuwa rais wa Wananchi. Ni wachache wetu tuliokuwa pale wakiwemo Mbunge wa Ruaraka TJ Kajwang na Miguna Miguna. Kitendo hiki cha ujasiri ndicho kilichangia Rais Uhuru Kenyatta kusalimiana na Bw Odinga,” akawaambia waombolezaji katika mazishi ya diwani wa zamani wa wadi ya Alego Kusini, Joshua Osuri.

Aliwashauri wakereketwa wa mchakato wa BBI kutovunjika moyo na wajiandae kupigia kura marekebisho yaliyomo kwenye mswada wa BBI kabla ya mwaka huu kutamatika.

“Nawataka mfahamu kwamba hakuna kizuri kinachopatikana kwa urahisi; sharti juhudi kubwa ziwekwe ilivyofanyika kabla ya kupatikana kwa Katiba ya sasa mnamo 2010,” Orengo akaeleza.

Aliwaomba wananchi kuwaombea wanapojiandaa kupinga uamuzi wa jopo la majaji watano wa Mahakama Kuu walioharamisha mchakato wa BBI wiki jana.

Seneta Orengo na Dkt Amollo wiki jana walishutumiwa vikali na wabunge wa ODM kutoka Luo Nyanza, wakiongozwa na Mbunge wa Ugunja Opiyo Wandayi, kwa madai kuwa walikaidi msimamo wa ODM Mswada wa BBI ulipojadiliwa katika Bunge la Kitaifa na Seneti.

Wawili hao pia walikuwa miongoni mwa jopo la mawakili waliotetea muungano wa NASA na Bw Odinga katika kesi ya kupinga ushindi wa Rais Kenyatta, katika Mahakama ya Juu, mnamo 2017.

Wakati huo huo, Katibu Mkuu wa ODM, Bw Edwin Sifuna amewataka mawaziri wanaotaka kujiunga na siasa wafanye hivyo badala ya kutumia vyombo vya usalama kutisha na kudhulumu wapinzani wao.

Akionekana kumrejelea Waziri wa Usalama wa Ndani, Dkt Fred Matiang’i, Bw Sifuna alimtaka kuingia siasa ikiwa anahisi kuwa na umaarufu katika ulingo huo.

You can share this post!

Bingwa wa ukaidi

Real Madrid wakamilisha kampeni za msimu huu wa 2020-21...