Michezo

Origi auzwe haraka iwezekanavyo, mashabiki wa Liverpool wasema

January 9th, 2019 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

MASHABIKI wa Liverpool FC wamekukosa subira na mshambuliaji Divock Origi, ambaye anamezewa mate na Fulham na Wolverhampton Wanderers, na wanataka auzwe katika kipindi hiki kifupi cha uhamisho cha Januari.

Hawajaficha hasira yao kwa Origi baada ya mchango wake kukosa kuwaepushia kichapo cha mabao 2-1 dhidi ya Wolverhampton Wanderers katika mechi ya Kombe la FA mnamo Januari 7, 2019.

Mbelgiji Origi, ambaye babake Mike Okoth alikuwa mshambuliaji mkali sana wa timu ya taifa ya Kenya, alifunga bao hilo la pekee la Liverpool katika dakika ya 51.

Raul Jimenez aliweka Wolves kifua mbele dakika ya 38 naye Ruben Neves akapachika bao la ushindi dakika nne baada ya Origi kuona lango.

Tovuti ya HITC inasema Origi hakuridhisha katika mechi hiyo ya raundi ya tatu. Imenukuu mashabiki kadhaa waliorushia Origi cheche za matusi baada ya mechi hiyo.

Aidha, gazeti la Daily Mirror limeripoti kwamba Wolves inataka Origi kwa karibu Sh2.6 bilioni. Ripoti zingine zinasema Fulham iko tayari kuipa Liverpool karibu Sh2 bilioni kupata huduma za Origi.