Origi awakomboa Reds tena

Origi awakomboa Reds tena

MILAN, ITALIA

Na MASHIRIKA

MBELGIJI Divock Origi alifuma wavuni kichwa kisafi Liverpool ikiandikisha historia kwa kuwa timu ya kwanza ya Uingereza kuvuna ushindi mara sita mfululizo kwenye mechi za makundi za Klabu Bingwa Ulaya, Jumanne.

Manchester City ilipoteza 2-1 dhidi ya Leipzig katika mechi ambayo beki Kyle Walker alilishwa kadi nyekundu, nao masupastaa Kylian Mbappe na Lionel Messi, walifunga mabao mawili kila mmoja Paris Saint-Germain wakachapa Club Brugge 4-1.

Real Madrid, Atletico Madrid, Ajax na Dortmund pia waling’ara Jumanne.Origi, ambaye babake alikuwa mshambuliaji matata wa Harambee Stars kati ya 1990 na 2004, alifunga bao la mwisho lililozamisha AC Milan 2-1 ugani San Siro.

Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 26, aliibuka mchezaji bora wa mchuano huo.Milan ilitangulia kutikisa nyavu za ‘Reds’ kupitia kwa Fikayo Tomori dakika ya 28. Hata hivyo, Liverpool ilijibu kupitia kwa mvamizi matata Mohamed Salah dakika ya 36 na Origi dakika ya 55 baada ya kipa Mike Maignan kutema makombora ya Alex Oxlade-Chamberlain na Sadio Mane mtawalia.

Goli la Origi la hivi punde lilipatikana siku chache baada pia ya kufunga la ushindi dhidi ya Wolves 1-0 dakika ya mwisho ligini.“Nadhani tulicheza vizuri sana. Sote tulitaka kuonyesha soka ya hali ya juu…,” alisema Origi ambaye nyota wa zamani wa Manchester United Rio Ferdinand amemlinganisha na Ole Gunnar Solskjaer na Javier Hernandez waliotegemewa sana wakitokea kitini.

Kocha Jurgen Klopp pia aliwasifu mabeki Nat Phillips na Ibrahima Konate kwa kazi nzuri ya katika mchuano huo kwa kuwazima washambuliaji wa Milan akiwemo gunge Zlatan Ibrahimovic.Liverpool imeungana na AC Milan, Paris Saint-Germain, Barcelona, Bayern Munich, Spartak Moscow, Real Madrid na Ajax katika orodha ya klabu pekee ambazo zimeshinda michuano yote sita ya makundi ya mashindano haya.

You can share this post!

Hii ndoto ya dereva chipukizi Yuvraj

Miheso aokoa Kenya Police, Homeboyz ikipaa kileleni mwa ligi

T L