Habari za Kitaifa

Orodha ya wanaolenga viatu vya Eric Theuri LSK yaongezeka

January 12th, 2024 2 min read

NA RICHARD MUNGUTI

KITI cha Urais wa Chama cha Wanasheria Nchini (LSK) kimeendelea kuwavutia wawaniaji huku wakili Peter Wanyama akijitosa kwenye kinyang’anyiro hicho.

Bw Wanyama aliwasilisha makaratasi yake ya uteuzi Alhamisi katika makao makuu ya LSK katika barabara ya Gitanga Road alisema wananchi wanahitaji mtetezi asiyetishika katika masuala ya kisheria.

Wakili huyo anayetazamia kumridhi rais wa sasa wakili Eric Theuri alisema wananchi wameumizwa mno na sheria zinazopitishwa na bunge na kuwaongezea msigo wa korti.

Akiwahutubia wanahabari baada ya kumkabidhi afisa msimamizi wa zoezi hilo katika afisi za LSK, Bw Wanyama alisema jukumu la kipekee la chama cha wanasheria ni kuhakikisha serikali haipitishi sheria zinazowabebesha wananchi mizigo mizito ya korti na sheria za kiimla.

Bw Wanyama ambaye uwaniaji wake kiti cha urais wa LSK uliidhinishwa na mawakili wenye tajriba ya juu Donald Kipkorir , Dancan Okatch , Danstan Omari , Shadrack Wambui miongoni mwa wengine amesema serikali kuu inapasa kuwajali wananchi wapato ya chini.

“Nachukua fursa hii kutahadharisha Rais William Ruto kwamba matamshi yake ya kushusha hadhi ya idara ya mahakama hayafai na anapasa kukoma mara moja,” Bw Wanyama alisema punde hati zake za uteuzi kuwania kiti hicho yalipokubaliwa na afisa msimamizi wa zoezi hilo.

Bw Wanyama alisema kuingiliwa kwa idara ya mahakama na ukandamizaji wa wananchi na kodi za kila uchao ni jambao linalopasa kupingwa vikali mahakamani na bungeni.

Wakili huyo alikosoa uongozi wa LSK akisema haujali maslaha ya maelfu ya mawakili wasio na ajira hata baada ya kuhitimu kuwa mawakili.

Uchaguzi huo wa LSK utakaofanywa February 29,2024 umewavutia wawaniaji watano wa kiti cha urais wa LSK.

Wengine waliowasilisha makaratasi yao ya uteuzi ni pamoja na Bi Carolyne Kamende Daudi (aliyekuwa naibu rais wa LSK wakati Bw Nelson Havi alipokuwa Rais wa LSK-2021), naibu rais wa sasa LSK Faith Odhiambo, Harriet Mboche na Bernard Ngetich.

Watano hawa wanatazamia kutwaa wadhifa huo baada ya muda wa Bw Theuri kuyoyoma Machi 2024.

Bw Theuri ndiye rais wa LSK wa 50 na atakayeshinda kiti hicho atakuwa wa 51.