Michezo

Orodha ya wanasoka wote bora Afrika

January 9th, 2019 2 min read

Na GEOFFREY ANENE

NYOTA Mohamed Salah ameibuka namba wani tena katika Tuzo za Shirikisho la Soka la Bara Afrika (CAF) baada ya kutawazwa Mwanasoka bora mwaka 2018 katika hafla ya kufana jijini Dakar, Senegal, Jumanne usiku.

Mshambuliaji huyu wa klabu ya Liverpool na timu ya taifa ya Misri aliwapiku Sadio Mane (Liverpool Senegal) na Mwanasoka bora wa Afrika mwaka 2015 Pierre-Emerick Aubameyang kutoka Gabon, ambaye anasakata soka yake ya malipo katika klabu ya Arsenal nchini Uingereza.

Watatu hawa walitajwa katika timu bora ya Afrika ya wachezaji 11. Wachezaji wengine waliojumuishwa katika ‘Africa Best XI’ ni kipa Denis Onyango (Uganda&Mamelodi Sundowns, mabeki Serge Aurier (Ivory Coast), Medhi Benatia (Morocco), Eric Bailly (Ivory Coast) na Kalidou Koulibaly () na viungo Naby Keita (), Thomas Partey (Ghana) na mwanasoka bora wa Afrika mwaka 2016 Riyad Mahrez (Algeria).

Salah, Aubameyang na Mane wanakamilisha orodha hiyo katika safu ya ushambuliaji.

Taji la Mwanasoka bora mwanamke liliponyoka Nigeria baada ya Chrestinah Thembi Kgatlana kutoka Afrika Kusini kutawazwa malkia. Aliibuka mfungaji bora na pia kung’ara sana katika dimba la Afrika (AWCON).

Afrika Kusini pia ilishinda taji la kocha bora wa mwaka wa timu ya kinadada kupitia kwa Desiree Ellis aliyeongoza nchi hiyo kupiga miamba Nigeria katika AWCON 2018 katika mechi za makundi kabla ya kupoteza dhidi ya wapinzani hawa katika fainali Desemba 1 nchini Ghana.

Kocha bora wa mwaka 2018 kwa upande wa wanaume ni Mfaransa Herve Renard anayenoa timu ya taifa ya Morocco. Mauritania, ambayo itashiriki AFCON kwa mara ya kwanza katika historia yake nchini Misri mwezi Juni na Julai mwaka 2019, ndiyo timu bora ya wanaume mwaka 2018 baada ya kupiku wanavisiwa wa Madagascar, ambao pia watakuwa AFCON kwa mara ya kwanza kabisa, na majirani wa Kenya, Uganda.

Itakumbukwa Harambee Stars ya Kenya ilikuwa katika orodha ya kwanza ya mataifa yaliyoteuliwa kuwania ubingwa wa kitengo hiki kabla ya kuondolewa mapema. Mabingwa wa soka ya kinadada ya Afrika, Super Falcons ya Nigeria walijiliwaza na taji la timu bora ya wanawake mwaka 2018.