Habari za Kaunti

Oscar Sudi bado yupo! Kilabu chake cha Timba XO kufunguliwa upya Agosti 7


MBUNGE wa Kapseret, Oscar Sudi, anatarajiwa kufungua tena klabu chake Timba XO mjini Eldoret baada ya sehemu hiyo ya burudani kuvamiwa na wahuni wakati wa maandamano ya kupinga serikali.

Kilabu hicho kinatarajiwa kufunguliwa upya mnamo Agosti 7, 2024.

Bw Sudi alieleza hayo wakati wa mahojiano na Obinna Live mnamo Ijumaa, Agosti 2.

Inasemekana kuwa watu wanaoshukiwa kuwa wahalifu waliharibu kuta za vioo, madirisha na milango ya kilabu hicho na kuiba pombe iliyogharimu mamilioni ya pesa wakati wa maandamano yaliyoongozwa na wanarika wa GenZ kupinga Mswada wa Fedha 2024.

Bw Sudi alifichua kuwa alipata hasara ya jumla ya Sh48 milioni.

“Nilitumia takriban Sh250 milioni kujenga Timba XO, Timba Hotel, na kila kitu. Ni bora kupoteza hiyo kuliko kuua watu,” alisema wakati wa mahojiano.

“Siku hiyo tungeua watu zaidi ya 50. Niliwaambia watu wangu wasimguse mtu yeyote, wakawaruhusu kufanya lolote wawezalo. Polisi walijaribu kadri ya uwezo wao ila wakashindwa. Sikuwa na ubaya kwani sikutaka watu wapoteze maisha,” akaongeza.

Mbunge huyo alisisitiza zaidi kwamba ingawa alipoteza kiasi kikubwa cha pesa, anashukuru kwamba hakuna mtu yeyote aliyepoteza maisha.

“Tukiweka gharama ya kila kitu, ikiwemo hoteli, nakadiria tulipoteza zaidi ya Sh48 milioni. Wahuni waliiba kila kitu lakini ni sawa, naomba walioiba vifaa vya Timba XO wavirudishe.”

Kufuatia tukio hilo, Sudi alisema zaidi ya wafanyakazi 220 katika klabu hicho walipoteza nafasi zao za kazi.

“Nililazimika kuwalipa kwa muda wa miezi miwili ili waweze kujikimu pamoja na familia zao,” alisema Bw Sudi.