Osoro atetea matamshi ya Naibu Rais kuhusu mfumo wa mashamba

Osoro atetea matamshi ya Naibu Rais kuhusu mfumo wa mashamba

NA SAMMY WAWERU

MBUNGE wa Mugirango Kusini Silvanus Osoro ametetea matamshi ya Naibu wa Rais, Rigathi Gachagua kuhusu mfumo wa mashamba.

Wiki iliyopita, Bw Gachagua alisema serikali itatoa mwelekeo kuruhusu wanaoishi karibu na misitu kufanya kilimo.

Akieleza kushangazwa kwake na Kenya kununua mahindi nje ya nchi ilhali ina mashamba ya kutosha, Naibu Rais alisema serikali itaibuka na mikakati wenyeji katika mazingira ya misitu wawe wakilima kati ya miti bila kuiharibu.

Maarufu kama Mfumo wa Mashamba, Bw Gachagua alisema utaiga nyayo za hayati Rais mstaafu Daniel Arap Moi.

Matamshi yake hata hivyo yamekosolewa na baadhi ya wanaharakati wa mazingira, wakisema mpango huo utachangia uharibifu wa misitu.

Kulingana na Osoro, kauli ya Naibu Rais ilitafsiriwa isivyofaa na kwamba yeye ni kiongozi wa hadhi ya juu Kenya anayejua thamani ya misitu.

“Wanaomkosoa, hawakuelewa alivyomaanisha. Ufahamu wangu, alinuwia lazima kuwe na mikakati maalum watakaoruhusiwa kufanya kilimo wasiharibu miti,” mbunge huyo akasema mapema Jumatatu.

Osoro hata hivyo alisema mpango huo utakapotolewa, amri itatoka kwa rais.

Wakati Gachagua akitoa matamshi hayo, Rais William Ruto alikuwa nje ya nchi.

Mwaka 2018, serikali ya Rais mstaafu Uhuru Kenyatta ilipiga marufuku ukataji wa miti katika misitu ya umma.

Dkt Ruto alikuwa Naibu wa Rais katika serikali ya mtangulizi wake, waliyoiongoza kati ya 2013 – 2022.

  • Tags

You can share this post!

Ruto aita wahubiri ikulu kwa maombi

Idadi ndogo ya wenyeji chuoni yamkera gavana

T L