Habari MsetoSiasa

Osotsi atimuliwa ANC

May 14th, 2019 1 min read

Na PETER MBURU

CHAMA cha ANC kinachoongozwa na Musalia Mudavadi Jumanne kilimtimua aliyekuwa Katibu wake Mkuu Godffrey Osotsi, siku chache tu baada ya kushindwa kutetea kiti chake cha Katibu Mkuu kortini.

Kupitia barua iliyotumwa na Katibu Mkuu wa chama hicho wa sasa Barrack Muluka Mei 14, Bw Osotsi alifahamishwa kuhusu kuondolewa kwake kuwa mwanachama wa ANC, siku moja tu baada ya Msajili wa Vyama vya Kisiasa kumwondoa kama Katibu Mkuu.

Kumekuwa na mizozo ya uongozi katika chama hicho cha Bw Mudavadi na Bw Osotsi alikuwa akipinga kuondolewa kwake kuwa Katibu Mkuu.

Hata hivyo, mahakama ilikubaliana na uongozi wa chama hicho kuwa Bw Osotsi anafaa kuondolewa kutoka wadhifa huo na Bw Muluka ambaye amekuwa na uungwaji mkono wa Bw Mudavadi akaidhinishwa rasmi.

Bado Bw Osotsi hajazungumza kuhusu hatua atakayochukua sasa, kwani kisheria mbunge akitimuliwa na chama ambacho alichaguliwa nacho anapoteza kiti cha ubunge.