Habari Mseto

Otiende Amollo aeleza kiini cha kuzirai mazishini

May 14th, 2018 1 min read

Na BENSON MATHEKA

MBUNGE wa Rarieda Otiende Amollo, Jumapili alifichua kilichomfanya azirai akihudhuria mazishi Kaunti ya Siaya Jumamosi iliyopita.

Kwenye ujumbe wa Twitter, mbunge huyo wa chama cha ODM alisema madaktari waligundua kwamba alikuwa na Malaria.

Hata hivyo, aliwaondolea hofu Wakenya akisema hali yake imeimarika.

“Sikujua kwamba Malaria inaweza kuwa hatari hivyo. Nilipata Malaria ambayo madaktari wamesema ilikuwa imeanza kuathiri ubongo! Kwa bahati nzuri, hali inashughulikiwa,” aliandika kwenye twitter.

Dkt Amollo alilazwa katika hospitali ya Aga Khan Hospital, Kisumu baada ya kuzirai akihudhuria mazishi eneo la Alego Usonga, Kaunti ya Siaya.

Alikuwa ameandamana na viongozi wengine seneta James Orengo, wabunge Samwel Atandi (Alego Usonga), Opiyo Wandayi (Ugunja) na Oburu Odinga (EALA) kumfariji aliyekuwa mbunge wa Alego Usonga, Peter Oloo Aringo kwa kufiwa na mwanawe Tom Gemma Aringo.

Alikimbizwa katika Bondo Medical Centre kwa huduma ya kwanza kabla ya kuhamishiwa Aga Khan Hospital, Kisumu.

Jumapili aliweka picha katika mitandao ya kijamii akiwa na jamaa zake akisema amepata nafuu baada ya kupata matibabu.

Mnamo Jumamosi Dkt Julius Okel, wa hospitali ya Aga Khan alisema mbunge huyo hakuwa hatarini.

Awali ilikisiwa kuwa Bw Amollo alizirai kutokana na uchovu.

Mnamo Alhamisi Mbunge huyo alihudhuria kikao cha kisikilizwa kwa kesi ya rufaa ya Gavana wa Homa Bay Cyrian Awiti mjini Kisumu.

Na Ijumaa alishinda katika eneo bunge lake akishiriki shughuli nyingi, ukiwemo mradi wake wa kuwajengea wajane makazi bora.