Otieno achanja pasi muhimu AIK ikizoa ushindi muhimu Ligi Kuu Uswidi

Otieno achanja pasi muhimu AIK ikizoa ushindi muhimu Ligi Kuu Uswidi

Na GEOFFREY ANENE

TIMU ya AIK anayochezea Mkenya Eric “Marcelo” Otieno iliweka hai matumaini yake finyu ya kushinda Ligi Kuu ya Uswidi baada ya kuchabanga wenyeji Elfsborg 4-2 ugani Boras Arena Jumatatu usiku.

Beki Otieno alichanja pasi kutoka pembeni kushoto iliyozalisha goli la mwisho la AIK kutoka kwa Nicolas Marcelo Stefanelli dakika ya 77.

Elsborg ilitangulia kuona lango kupitia kwa Rasmus Alm alipomwaga kipa Kristoffer Nordfeldt dakika ya 12.

Nabil Bahoui alisawazisha 1-1 kupitia kichwa dakika ya 27 baada ya kona kupatikana.

Hata hivyo, Elfsborg ilifurahia kuenda mapumzikoni ikiongoza 2-1 baada ya Alm kufuma wavuni goli la pili dakika ya 41.

AIK ilirejea kipindi cha pili na ari ya kuepuka kipigo. Filip Rogic alifanya mabao kuwa 2-2 dakika ya 54 kupitia shuti kali kutoka nje ya kisanduku baada ya beki wa Elfsborg kuondoa pasi hatari vibaya.

Timu ya AIK ilipata kuongoza mechi hiyo kwa mara ya kwanza dakika mbili baadaye baada ya Stefanelli kutikisa nyavu mabeki walipozembea kuondosha kombora lililokuwa limegonga mwamba.

Otieno kisha alisuka pasi iliyokamilisha kwa ustadi na Stefanelli. Mchezaji wa AIK, Henok Goitom, 37, alitangaza kustaafu baada ya mechi hiyo iliyosakatwa mbele ya mashabiki 10, 157.

AIK inakamata nafasi ya pili kwenye ligi hiyo ya klabu 16 kwa alama 56 baada ya kujibwaga uwanjani mara 29.

Viongozi Malmo wana alama 58. Ligi hiyo itatamatika Desemba 4, huku AIK ikialika nambari 10 Sirius ugani Friends Arena nayo Malmo itavaana na nambari 13 Halmstad. Mshindi ataingia mechi za kufuzu kushiriki Klabu Bingwa Ulaya naye nambari mbili atawania tiketi ya kushiriki Ligi ya Uropa.

You can share this post!

Watu 7.1 milioni wamepata chanjo dhidi ya corona kufikia...

Mikakati ya serikali ilinusuru Kenya kwa corona –...

T L