Michezo

Otieno akwezwa cheo FKF huku Muthomi akichunguzwa

July 23rd, 2019 2 min read

Na CELLESTINE OLILO

KATIKA juhudi za kukabiliana na sifa mbaya inayotishia uongozi wake, Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) limepandisha cheo Afisa wa Mawasiliano na Mauzo Barry Otieno kuwa kaimu Afisa Mkuu Mtendaji.

Tangazo hili lilifanywa siku moja baada ya Afisa Mkuu Mtendaji Robert Muthomi, ambaye anachunguzwa kwa madai ya kujaribu kusukuma uhamisho wa mshambuliaji John Avire akiwa bado na kandarasi na Sofapaka FC, kukaa kando akisubiri uamuzi wa Kamati ya Nidhamu ya FKF.

“Robert Muthomi ameomba kukaa kando kutoka wadhifa wake na tumekubali ombi lake, tukitumai kwamba hatimaye madai haya yataondolewa.

“Kamati ya dharura ya FKF ilikutana jana na kuamua kuwa Mkuu wa Mawasiliano Barry Otieno ashikilie wadhifa wa Afisa Mkuu Mtendaji kwa muda wakati Robert hayupo kwa sababu lazima FKF iendelee na majukumu yake,” alisema Rais wa FKF, Mwendwa, ambaye aliongeza kuwa kamati hiyo itatoa uamuzi wake kuhusu Muthomi kwa kati ya siku 30 na 35 zijazo.

Kwa Otieno, cheo kipya kitaimarisha wasifukazi wake kwa sababu kinamuinua kutoka kazi ya kukabiliana na matamshi ya umma ya Mwendwa na kumfanya kuwa afisa wa tatu kwa mamlaka katika orodha ya viongozi wa shirikisho hili.

Katika majukumu yake mapya kama mmoja wa viongozi wakuu wa shirikisho, Otieno atashuhudia maslahi yakiboreshwa ikiwemo usafiri wa mara kwa mara barani Afrika kuwakilisha shirikisho, na kutoa uamuzi muhimu kwa niaba ya shirikisho.

Mambo ni tofauti na magumu kwa Muthomi.

Kwanza, atatumai ataondolewa madai hayo yanayotia doa sifa yake. Akirejeshwa kazini, atalazimika kufanya kazi maradufu ili kurejesha uaminifu na uungwaji mkono aliopoteza.

Akitangaza uamuzi wa kamati ya dharura ya FKF katika kikao cha Jumatatu na wanahabari jijini Nairobi, Mwendwa ambaye aliandamana na naibu wake Doris Petra, alionekana mtu aliye na huzuni.

Wandani wake wanasema kuwa uamuzi wa kumwondoa Muthomi kutoka afisi yake, na kuteua Otieno, uliafikiwa baada ya mashauriano ya kina yaliyokamilika usiku.

Supa

Uhusiano wa Muthomi na Mwendwa ulianza miaka kadhaa iliyopita walipokuwa wasimamizi wa klabu katika Ligi ya Supa, ambayo ni ligi ya daraja la pili.

Muthomi alikuwa mwenyekiti wa Nakuru All Stars, naye Mwendwa alikuwa Kariobangi Sharks akihudumu kama Afisa Mkuu Mtendaji, na pia afisa wa kuweka rekodi za wanasoka nchini Kenya.

Waliingia FKF mwaka 2016 kuchukua uongozi kutoka kwa Sam Nyamweya, ambaye alijiondoa kwenye uchaguzi siku moja kabla ya kura kupigwa.

Uhusiano huu unaonekana kuharibika wakati mbaya, hasa kwa sababu Mwendwa ametangaza kuwa atawania tena Novemba mwaka huu.

Ijumaa iliyopita, FKF ilithibitisha kuwa imeanza kuchunguza Muthomi, ambaye alikuwa amekiri kuandikia Ubalozi wa Misri barua kuuomba umpe Avire kibali cha kusafiri. Hii ilikuwa siku nane tu baada ya mshambuliaji huyu, ambaye kandarasi yake na Sofapaka itatamatika Desemba mwaka 2020, alikuwa nchini Misri akichezea Kenya kwenye Kombe la Afrika (AFCON).