Otieno arejea kutoka Zambia kuwa kizibo cha Asieche kambini mwa Sofapaka

Otieno arejea kutoka Zambia kuwa kizibo cha Asieche kambini mwa Sofapaka

Na CHRIS ADUNGO

KOCHA wa Sofapaka, Ken Odhiambo, anaamini kwamba kutua kwa mvamizi Timothy Otieno kambini mwao sasa kunaweka hai matumaini yao ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Kenya (FKFPL) msimu huu.

Otieno ambaye ni fowadi wa Harambee Stars ameingia katika sajili rasmi ya Batoto ba Mungu waliotawazwa wafalme wa Ligi Kuu mnamo 2009 baada ya kutamatisha ghafla mkataba wake wa miaka miwili na Napsa Stars ya Zambia iliyomtwaa kutoka Tusker FC mnamo Septemba 2020.

“Ni mshambuliaji tegemeo anayeleta uzoefu mpana, tajriba pevu na sifa za uongozi kikosini. Ni matarajio yetu kwamba atakuwa kielelezo kwa chipukizi wengi na kuja kwake kutainua viwango vya ushindani na kuimarisha makali yetu kwenye safu ya mbele,” akasema kocha huyo wa zamani wa Bandari FC.

Hadi alipokatiza uhusiano wake na Tusker na kuyoyomea Zambia, Otieno alikuwa akiongoza orodha ya wafungaji bora wa FKFPL mnamo 2019-20 kwa mabao 14.

Kwa mujibu Odhiambo, huenda usimamizi wa Sofapaka ukampokeza Otieno utepe wa unahodha baada ya kikosi hicho kuagana rasmi na kigogo Elli Asieche.

“Asieche ambaye aliteuliwa kuwa kapteni wetu mwanzoni mwa msimu huu ameagana nasi. Tunamtakia kila la heri,” ikasema sehemu ya taarifa iliyotolewa na Batoto ba Mungu.

Katika kipindi cha miaka minane ya kuhudumu kwake kambini mwa Sofapaka, Asieche aliwavunia waajiri wake hao makombe manne – GOtv Shield Cup, DSTV Super Cup na mataji mawili ya Charity Cup.

  • Tags

You can share this post!

Wanaojiita ‘mahasla’ kusukumwa jela

Gor Mahia kusajili wanasoka wawili zaidi wa kigeni