Michezo

Ozil kuuzwa mwishoni mwa msimu

June 20th, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

INGAWA Mesut Ozil anatazamia kusalia uwanjani Emirates hadi mkataba wake utakapotamatika rasmi c wa 2020-21, Arsenal wamefichua azma ya kumtia kiungo huyo mnadani mwishoni mwa msimu huu.

Chini ya kocha Mikel Arteta, Arsenal wanakabiliwa na ulazima wa kukisuka upya kikosi chao kutokana na uchechefu wa fedha ambao umechangiwa na janga la corona na pigo la kukosa kushiriki kipute cha Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) kwa msimu wa nne mfululizo.

Arsenal wameshikilia kwamba watamuuza Ozil ili mshahara wake wa Sh49 milioni kwa wiki na fedha zitakazopatikana kutokana na mauzo yake zimwezesha Arteta kujinasia huduma za chipukizi wengi wa bei rahisi watakaoongoza ufufuo wa makali ya klabu.

Japo Arsenal walikuwa radhi kuzinadi huduma za kiungo huyo mzawa wa Uturuki na raia wa Ujerumani msimu uliopita wa 2018-19, hakuna mnunuzi yeyote aliyejitokeza kutokana na ukubwa wa gharama ya kumdumisha kimshahara.

Ozil, 31, alijipata katika uhusiano uliotawaliwa na mvurugano mkubwa kati yake na kocha Unai Emery aliyetimuliwa mwishoni mwa mwaka 2019 na nafasi yake kutwaliwa na mkufunzi Arteta mwezi mmoja baadaye.

Chini ya Arteta, Ozil alipangwa katika kikosi cha kwanza cha Arsenal katika jumla ya mechi 10 za EPL kabla ya soka ya Uingereza kusitishwa kwa muda kutokana na janga la corona mnamo Machi 13, 2020. Ingawa hivyo, aliachwa nje ya kikosi kipana cha wanasoka 20 ambao Arteta alipania kuwategemea dhidi ya Manchester City waliowapiga 3-0 uwanjani Etihad. Isitoshe, Ozil hakuwajibishwa katika mchuano ulioshuhudia Arsenal wakizabwa 2-1 na Brighton mnamo Juni 20 uwanjani Sussex.

Ozil ndiye mchezaji wa pekee wa kikosi cha Arsenal aliyekataa kupunguziwa mshahara kwa hadi asilimia 12.5 baada ya Arteta kuwasilisha pendekezo hilo mnamo Aprili katika juhudi za kukabiliana na janga la corona.

Ozil aliyejiunga na Arsenal kutoka Real Madrid kwa kima cha Sh5.9 bilioni mnamo 2013, sasa anawaniwa na Fernabahce ya Uturuki.

Mnamo Mei 2020, Ozil alipania kuzima tetesi zilizokuwa zikimhusisha na uwezekano wa kubanduka Arsenal kwa kufichua kwamba atasalia ugani Emirates kwa muhula mwingine mmoja.

Hayo yalikuwa kwa mujibu wa wakala wake Erkut Sogut ambaye ameshikilia kwamba mteja wake huyo hana mipango yoyote ya kuagana na Arsenal hivi karibuni.

Awali, Ozil alikuwa akitarajiwa kujiunga na Fenerbahce ya Uturuki mwishoni mwa msimu huu baada na rafikiye Acun Ilicali ambaye ni mtangazaji wa Turkish TV kutangaza kuwa Ozil amemweleza awaandae kisaikolojia mashabiki wa Ligi Kuu ya Uturuki kwamba atakuwa akinogesha kipute hicho katika msimu wa 2021-22.