Michezo

Ozil ni mchawi wa gozi – Iwobi

October 23rd, 2018 1 min read

Na CECIL ODONGO

NYOTA wa Arsenal Alex Iwobi amekubali kwamba ni hidaya kwake kucheza pamoja na Mesut Ozil baada ya Mjerumani huyo kutandaza soka ya hali ya juu na kuisaidia Arsenal kusajili ushindi kwa mara ya 10 mfululizo katika ligi ya Uingereza na wa mabao 3-1 mechi dhidi ya Leicester Jumatatu Oktoba 22 ugani Emirates.

Ozil alikuwa moto wa kuotea mbali wakati wa mtanange huo na hata alifunga bao la kwanza la ‘The Gunners’ baada ya ushirikiano wa kupigiwa mfano kati yake na raia wa Gabon Pierre-Emerick Aubameyang ambaye pia alitia wavuni mabao mawili.

“Ni bahati kwamba mie hucheza naye kila siku. Tumekuwa tukishiriki mazoezi ya pamoja naye tangu nikiwa na miaka 17 hadi leo na nimeona maajabu ya soka anayoyaweza kuyafanya. Kwa kweli amejaaliwa kipaji aula na alidhihirisha hayo wakati wa mechi  ya Leicester,” akasema Iwobi.

Mshambulizi huyo alitwikwa mkoba wa unahodha kwa mara ya kwanza na kwa kweli aliongoza kwa mfano wakati  mechi yote kwa kusakata soka ya kuvutia.

Iwobi ambaye ni kiungo mkabaji vile vile alikuwa wembe na akafichua siri kwamba Ozil ndiye humpa maelekezo na msukumo wa kutamba kila wakati.

“Yeye hunishajiisha kwa mawaidha ke kem na mzaha ila kila mara huniambia naweza kuwa mchawi zaidi wa soka kuliko jinsi nilivyo kwa sasa. Yeye ni kiungo muhimu sana kwangu na wenzangu timuni,” akasema Iwobi.