PAA yajipata pabaya Jumwa akikaa ngumu

PAA yajipata pabaya Jumwa akikaa ngumu

VALENTINE OBARA NA PHILIP MUYANGA

CHAMA cha Pamoja African Alliance (PAA) kinachoongozwa na Gavana wa Kilifi, Bw Amason Kingi, kinapitia hali ngumu baada ya kile cha United Democratic Alliance (UDA), kuteka mikutano ya hadhara ya muungano wa Kenya Kwanza iliyofanywa kaunti za Pwani.

Mbali na PAA kukosa kujipa nguvu katika mikutano hiyo iliyoongozwa na Naibu Rais William Ruto anaayesimamia UDA, jopo la kusikiliza malalamishi kuhusu vyama vya kisiasa, pia lilitupa nje ombi la chama hicho kutaka kuondoka katika Muungano wa Azimio la Umoja One Kenya.

Dkt Ruto alianza ziara zake Pwani mnamo Jumanne katika Kaunti ya Taita Taveta, kabla kuzuru Kaunti za Mombasa na Kilifi.

Ijapokuwa Bw Kingi alipewa nafasi mbele katika mikutano hiyo kwa msingi wa kuwa kwenye kikosi cha vinara wa Kenya Kwanza eneo la Pwani, ilidhihirika wawaniaji viti kupitia chama chake, watakabiliwa na ushindani mkali kutoka kwa UDA katika kampeni za pamoja za Kenya Kwanza.

Wakati wa mikutano hiyo, Dkt Ruto na Gavana wa Kwale, Bw Salim Mvurya, waliongoza wanachama wengine wa UDA waliokuwepo kupigia debe wawaniaji viti kupitia kwa chama hicho.

Waliopigiwa debe zaidi ni wawaniaji ugavana ambao ni aliyekuwa seneta wa Mombasa, Bw Hassan Omar (Mombasa), Mbunge wa Malindi, Bi Aisha Jumwa (Kilifi), na Naibu Gavana wa Malindi, Bi Fatuma Achani (Kwale).

Naibu Gavana wa Mombasa, Dkt William Kingi ambaye ndiye mwaniaji ugavana Mombasa kupitia PAA, hakuhudhuria mkutano wa Kenya Kwanza uliofanywa Jumatano, huku Bw George Kithi, anayewania cheo hicho dhidi ya Bi Jumwa, akikosa kujipigia debe ipasavyo katika mkutano wa muungano huo Kilifi.

Bi Jumwa hakuficha nia yake kutaka kuachiwa nafasi ya kupeperusha bendera ya Kenya Kwanza kwa kinyang’anyiro cha kurithi kiti cha Gavana Kingi.

“Hii Kilifi hatuwezi kuiacha iende kwa Azimio. Mtafutieni kazi kijana George Kithi na ugavana wa Kilifi ubaki na Aisha Jumwa. Nilishaomba na ninaomba tena, Gavana Kingi anipe kura yake,” akasema Bi Jumwa.

Kiti hicho kinamezewa mate pia na aliyekuwa waziri msaidizi wa ugatuzi, Bw Gideon Mung’aro, ambaye ni mwanachama wa ODM kilicho ndani ya Azimio.

Bw Kingi alipoongoza PAA kujiondoa katika Azimio ili kuingia Kenya Kwanza, Dkt Ruto alikuwa ameahidi kutakuwa na mashauriano ili wakubaliane kuhusu baadhi ya viti ambavyo wawaniaji wa vyama hivyo viwili wanaweza kuachiana.

Hata hivyo, uamuzi wa jopo la kutatua mizozo ya vyama vya kisiasa huenda ukatatiza mpango huo.Bi Josephine Wairimu Kinyanjui, ambaye ni mwanachama wa PAA, alikuwa amedai kuwa chama hicho kilisajiliwa kimakosa kama chama tanzu cha Azimio kwani wanachama walitaka kujiunga na muungano wa vyama wala si chama cha muungano.

Jopo hilo lilisema haliwezi kuendelea kusikiliza malalamishi hayo kwa vile Bi Kinyanjui hakuthibitisha juhudi zozote zilifanywa kutatua malalamishi yao ndani ya Azimio kabla kuelekea kwa jopo la kutatua mizozo ya vyama vya kisiasa.

  • Tags

You can share this post!

MAWAIDHA YA KIISLAMU: Uaminifu ndio upeo wa imani ya mja wa...

Wasafiri wataka ujenzi wa Uwanja wa Ndege Manda ukamilishwe

T L