PAC yatisha kukatiza pesa za mashirika, wizara ambazo wakuu wake watafeli kufika mbele yake

PAC yatisha kukatiza pesa za mashirika, wizara ambazo wakuu wake watafeli kufika mbele yake

NA CHARLES WASONGA

KAMATI ya Bunge kuhusu Uhasibu (PAC) sasa inataka Wizara, Idara na Mashirika ya Serikali (MDAs) yanayoongozwa na maafisa wanaofeli kufika mbele yake kujibu maswali kuhusu matumizi ya fedha, yanyimwe ufadhili kutoka Hazina ya Kitaifa.

Mwenyekiti wa kamati hiyo John Mbadi amesema wakati umewadia kwa Bunge la Kitaifa kuwa makini kuhakikisha kuwa asasi za umma zinawajibikia fedha zilizotengewa katika bajeti ya kitaifa.

“Kuanzia sasa wizara ambazo zitakaidi agizo la PAC kufika mbele yake kuwajibikia pesa zilizotengewa zitanyimwa mgao wa fedha kutoka Hazina ya Kitaifa. Tutawasilisha pendekezo hili bungeni kwa sababu sheria inaturuhusu kufanya hivyo,” akasema Mbunge huyo Maalum.

Bw Mbadi alitoa onyo hilo Jumatano baada ya Katibu katika Wizara ya Fedha Chris Kiptoo kufeli kufika mbele ya PAC kujibu maswali 47 yaliyoibuliwa na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kuhusu matumizi ya fedha za umma katika wizara yao katika miaka ya kifedha ya 2020/2021.

Lakini katika barua aliyomwandikia Karani wa Bunge la Kitaifa Samuel Njoroge, Dkt Kiptoo aliomba mkutano wa maafisa wa Wizara ya Fedha na PAC uahirishwe hadi siku nyingine, ombi ambalo liliwakera wanachama wa kamati hiyo.

Wabunge wanachama wa PAC walisema sababu aliyotoa Dkt Kiptoo “haina msingi wowote.”

“Kwa sababu nimebanwa na shughuli za kikazi, ninaomba kamati ya PAC itenge tarehe na siku nyingine ambapo maafisa wa Wizara ya Fedha watafika mbele ya kamati hiyo, kutoka Februari 8 hadi Februari 21, 2023,” ikasema sehemu ya barua hiyo iliyowasilishwa na Bw Mbadi kwa PAC.

Lakini Mbadi alisema kamati yake haitakubali maombi ya mashahidi wa kuitaka ibadilishe tarehe ya mashahidi kufika mbele ya kamati hiyo kwa sababu maombi kama hayo yanaathiri “utendakazi wa PAC.”

“Wizara za serikali sharti ziwe tayari kuwajibikia pesa zilizotengewa kutoka mfuko wa umma. Ikiwa haziko tayari kuwajibikia pesa hizo hivyo hazipasi kutengewa pesa zaidi,” akasema Bw Mbadi.

Mbunge huyo maalum alisema tayari PAC imeandaa ratiba ya vikao vya kuchunguza taarifa za matumizi ya fedha katika wizara na mashirika mbalimbali kwa kipindi cha miezi mitatu.

“Kwa hivyo, hatutaruhusu mchakato huu kucheleweshwa na hivyo tunahimiza maafisa wote walioalikwa kufika bila kuchelewa,” Bw Mbadi akasisitiza.

Kauli hiyo iliungwa mkono na Mbunge wa Lugari Nabii Nabwera, ambaye alisema PAC iliipa Wizara ya Fedha muda wa kutosha kuwasilisha majibu yake.

“Kwa kufeli kufika mbele yetu, maafisa hawa wanaonyesha dharau kwa kamati hii,” akasema.

Hata hivyo, kamati hiyo iliamua kwamba Dkt Kiptoo afike mbele yake mnamo Februari 16 na sio mnamo Februari 21 alivyoomba.
  • Tags

You can share this post!

Kunguni waongezeka katika lojing’i Kisumu

TANZIA: Huzuni baada ya mchezaji nyota wa Tong-IL Moo-Do...

T L