Habari Mseto

Pacha aliyeibwa hospitalini Kenyatta apatikana

February 21st, 2018 2 min read

Picha ya mnaso kwa video yaonyesha mamaye pacha hao akisema na wanahabari Februari 20, 2018. Picha/ Maktaba

Na PETER CHANGTOEK na BERNARDINE MUTANU

MTOTO pacha aliyeibwa katika Hospitali Kuu ya Kenyatta alipatikana Jumanne, na mshukiwa kukamatwa eneo la Kawangware, Nairobi.

Mtoto huyo, Prince, aliyeibwa Jumapili KNH, eneo la kungoja kuhudumiwa, alipatikana Kawangware 56 baada ya umma kumfahamisha babake, Job Nyatiti Ouko.

Babake mtoto huyo wa majuma mawili, jana alithibitisha kumpata mwanawe, nyumbani mwa mama huyo.

Bw Ouko alikuwa amempeleka mkewe katika KNH akiwa na matatizo ya moyo na kuwabeba pacha wake wa wiki mbili, ila hakujua angekabiliwa na masaibu zaidi.

Wakati wa mahojiano, Bw Ouko alisema, “Nilipigiwa simu na mtu aliyenifahamishwa kuwa aliona mwanamke aliyefanana na aliyeonyeshanwa katika video ya CCTV eneo la Kawangware. Aliniambia kuwa hakuwa akinyonyesha mtoto aliyekuwa naye.”

Kulingana na baba huyo, walimfumania mwanamke huyo akitaka kuondoka mtaani. Kabla ya kumpata, alikuwa amefanya mahojiano katika runinga moja ya humu nchini.

Ni baada ya dakika 30 baada ya mahojiano hayo alipopigiwa simu na kufahamishwa kuhusiana na kupatikana kwa mtoto huyo.

“Ni kupitia kwa mahojiano hayo ambapo nilipigiwa simu baada ya dakika 30 na jirani wa mshukiwa,’’ alisema.

Baada ya kufahamishwa, Bw Ouko alitafuta chifu wa eneo hilo ambaye aliandamana naye pamoja na maafisa wa polisi kutoka kambi ya polisi wa utawala, Kawangware, hadi nyumbani mwa mshukiwa huyo.

 

Nusura auawe

Mtuhumiwa, aliyenusurika kuuliwa na umma uliokuwa na ghadhabu, alipelekwa katika kituo cha polisi cha Muthangari kabla ya kuhamishiwa Kituo cha Polisi cha Kilimani.

Iliwabidi maafisa wa polisi kuwatawanya watu waliopania kumpiga mwanamke huyo, kabla ya kumpandisha kwa gari lao huku akilia.

Mtoto alipewa babake, aliyempeleka KNH ili aweze kuhudumiwa kimatibabu.

Mamake watoto hao, Jane Kerubo, ambaye alijifungua wiki mbili zilizopita KNH alikuwa amerejeshwa humo Jumapili saa nane asubuhi kwa uchunguzi zaidi baada ya kuugua.

Kamera za CCTV KNH zilimnakili mwanamke aliyeshukiwa kuiba mtoto huyo, dakika chache kabla ya kupanda bodaboda na kutokomea.

Inaaminika kuwa Bw Ouko na mkewe walianza kuzungumza na mwanamke huyo aliyekuwa ameandamana na mwanamke mwingine, kwa sababu walikuwa wakiongea lugha ya kwao, na ndiposa wakawaachia watoto wao kuwaangalilia.

Baada ya muda mfupi, mmoja wa wanawake alikimbia chumbani walimokuwa na kuwafahamisha kuwa mwanamke yule mwingine alikuwa ametoroka na mtoto mmoja.