Michezo

Pacman sasa aomba kulimana tena na Moneyman

January 23rd, 2019 1 min read

MASHIRIKA Na PETER MBURU

MIAKA mitatu baada ya wanamasumbwi Manny Pacquiao (Pacman) na Floyd Mayweather (Moneyman) kushiriki kwa “pigano la karne”, Bw Pacquiao sasa anataka pigano jingine kuandaliwa, ili ajitetee uwanjani kuhusu kushindwa kwake mnamo 2015.

Baada ya kutetea taji lake la WBA katika pigano la Jumamosi, mpiganaji huyo wa Ufilipino alimpa changamoto mshindi wa mara tano katika mapigano ya dunia, Mayweather kuwa waandaliwe pigano la marudio.

Bw Pacquiao ana miaka 40, naye Mayweather 41.

Bw Mayweather ambaye alistaafu alikuwa katika uwanja wa pigano huko Las Vegas akijitazamia wakati Pacquiao alimshinda mpiganaji wa Marekani AAdrien Broner kwa ushindi wa pamoja.

Akizungumza na vyombo vya habari baada ya pigano, Pacquiao aliulizwa tena na tena kuhusu uwezekano wa kupigana na Mayweather tena.

“Ujumbe wangu ni kuwa bado niko imara na ikiwa atarejea uwanjani akitaka kunikabili, mimi ni shujaa. Akitaka arejee uwanjani na tutapigana tena,” Pacquiao akasema.

“Ikiwa anataka kurejea kutoka kustaafu, atangaze na anialike. Mimi ni shujaa na sichagui wa kukabiliana naye. Nasubiri tu kuona atakayenikabili, atakayetaka taji langu,” akasema.

Pigano la Pacquiao na Mayweather mnamo 2015 lilivutia watazamaji wengi, tiketi zake zikilipishwa hadi Sh3.5milioni na waliotazama kwa televisheni hadi Sh10,000. Pigano hilo limesifiwa kuwa kali zaidi katika historia ya mchezo wa dondi.

Hata hivyo, ijapokuwa majuzi Mayweather alirejea uwanjani na kutumia sekunde 140 kumpiga mwanabondia kutoka Japan Tenshin Nasukawa katika pigano la siku moja kabla ya kuvuka mwaka, meneja wake Leonard Ellerbe alieleza wanahabari kuwa mpiganaji huyo hana haja na kupigana na Pacquiao.

Baada ya pigano hilo, alisema “kila wakati sio kuhusu pesa tu. Ni kipi kingine anaweza kufanya? Hana haja wala mapenzi kwa sasa.”

Alisema mpiganaji huyo sasa anashughulika na maisha mengine kama kutalii na kuendesha biashara zake, akila pesa nyingi alizopata wakati akiwa kazini.

Hata licha ya pigano na Nasukawa, Mayweather alisisitiza kuwa bado amestaafu, akisema pigano lilikuwa la kufurahisha mashabiki tu.