Habari Mseto

Padre alaumiwa waumini kushambulia wanahabari

December 12th, 2020 2 min read

Na MASHIRIKA

LAGOS, Nigeria

PADRE maarufu wa Kanisa Katoliki nchini Nigeria, Father Ejike Mbaka na baadhi ya washiriki wa kanisa lake waliwashambulia wanahabari wa BBC waliokuwa wakisubiri kumhoji nyumbani kwake mjini Emene, Kusini Mashariki mwa jimbo la Enugu.

Kisa hicho kilitokea Jumatano wakati wanahabari Chioma Obianinwa, Nnamdi Agbanelo na dereva wao Ndubuisi Nwafor, waliokuwa wameandamana na Padre mwingine, Cajethan Obiekezie na msaidizi wake, Solomon Orakam walipoenda katika kanisa la Mbaka la Adoration Ministry kumhoji.

Padre Obiekezie alikuwa amepanga na wanahabari hao wamhoji Mbaka, lakini walipofika katika kanisa lake walipata akihubiri.

Padre Obiekezie, aliwapeleka wanahabari hao katika boma la Padre Mbaka ili wamhoji baada ya kumaliza kuhubiri.

Kulingana na BBC, Padre Mbaka alipofika nyumbani, wanahabari hao walikuwa wakimsubiri kwenye gari lao na Padre Obiekezie alitoka kwenda kuzungumza naye. Ni wakati huo ambapo walizingirwa na wanaume wapatao 20.

Wanaume hao waliwapokonya vifaa vyao na wakatisha kuwaua wakiwalaumu kwa kuandika habari mbaya kumhusu Mbaka.

“Mbaka alituambia tusubiri amalize kuhubiri tumhoji. Wanaume waliokuwa nje ya nyumba yake walisema BBC Igbo huandika mambo mabaya kumhusu Mbaka. Walianza kuwapiga Nnamdi, Solomon na Ndubuisi. Walitupiga vibaya na kila mmoja wetu alipata majeraha ya kichwani na mwili wote,” Obianinwa alisema.

Alisema kwamba, Padre Mbaka na Obiekezie walitoka nje ya nyumba waliposikia kelele na Mbaka akamdunga kidole usoni akimuita shetani, kitendo ambacho kiliwachochea wanaume hao kuendelea kuwapiga vikali huku kasisi huyo akiendelea kuwafokea na kuwatusi.

Mwanahabari huyo alisema Mbaka aliagiza wanaume hao kuwapokonya simu na kamera zao.

“Walijaribu kumnyonga T Nnamdi. Padre Obiekezie alikuwa akiwaambia waache kutupiga lakini walimshambulia pia na kumpokonya simu yake,” alisema.

Kulingana na Obianinwa waliacha kuwapiga alipopiga nduru akilia kuwa dunia itajua kwamba waliuliwa katika nyumba ya Mbaka.

Ni wakati huo ambapo Padre Mbaka aliwaagiza waondoke kabla ya wanaume hao kuwaua. Aliwaambia wanaume hao kuwarudishia wanahabari hao kamera zao kisha akawafukuza. Wanaume hao waliwafuata hadi wakahakikisha waliondoka jimbo hilo wasiripoti kwa polisi au kwenda hospitali humo.

BBC iliripoti kuwa simu ambayo Padre Mbaka hutumia kuwasiliana na wafuasi wake ilizimwa baada ya kisanga hicho.