Habari Mseto

‘Paka Mzee’ Pennant ajinasia mpenzi mpya baada ya kutemana na mkewe

February 17th, 2024 2 min read

NA CHRIS ADUNGO

MWANASOKA wa zamani wa Arsenal na Liverpool, Jermaine Pennant, amejinasia mrembo mpya wiki mbili tu baada ya mkewe kumtema.

Mkongwe huyo, 41, alinaswa na kamera wiki hii akishiriki chamcha na mwigizaji maarufu nchini Uingereza, Charlotte Kirk, 31, ambaye pia alikuwa ameandamana na jibwa lake.

Japo ilikuwa mara ya kwanza wawili hao kuonekana peupe, inaaminika wamekuwa wakiwasiliana na kutumiana picha na video mitandaoni.

Kwa mujibu wa gazeti la The Sun, “Jermaine alianza kumtambalia Charlotte kimapenzi zaidi ya miezi minne iliyopita na uhusiano huo ndio ulichangia kusambaratika kwa ndoa ya sogora huyo na mkewe Jess Impiazzi.”

“Kuanza kuonekana hadharani jijini London ni ishara ya kukomaa kwa penzi lao. Tusubiri makuu zaidi kwa sababu sawa na Charlotte, lengo la Jermaine pia ni kupata jiko.”

Jermaine alitemana na Jess, 34, mnamo Desemba 2023 baada ya michepuko yake kufichuka.

Aliamriwa kuondoka nyumbani kwa mrembo huyo ambaye pia ni mwanahabari mnamo Januari mwaka huu.

Wakati huo huo, kichuna Bruna Marquezine ametangaza kuwa jeraha la moyoni aliloachiwa na Neymar Jr aliyemtema kama chingamu mnamo 2018 sasa limepona kabisa na yuko radhi kupenda tena.

Marquezine wakati walikuwa wapenzi. PICHA | MAKTABA

Kidosho huyo mwenye umbo la tausi alitumia Instagram kufichua hayo wiki hii na ujumbe aliopakia kwenye mtandao huo wa kijamii ukasomwa na zaidi ya mashabiki milioni 1.4 katika kipindi cha saa 24.

Chini ya picha yake akiwa amevalia rinda dogo la rangi nyeusi, mrembo huyo aliandika: “Niko katika hali shwari kabisa kihisia kurejea sokoni kusaka hifadhi mpya ya penzi langu.”

Alipoulizwa na wadaku iwapo ana mpango wa kurudiana na Neymar aliyeachwa na kipusa Bruna Biancardi mwishoni mwa mwaka jana kwa sababu ya jicho kali la nje, Marquezine alikana upesi.

“Sioni kabisa uwezekano wa hilo kufanyika. Ndiye aliyenitema baada ya kuishi naye kuanzia 2012. Ni zaidi ya miaka mitano sasa imepita tangu tuwasiliane na sijawahi kuhisi chochote cha kutuunganisha tena.”

Marquezine, 28, anajivunia zaidi ya wafuasi milioni 45 kwenye Instagram na chapisho lake la wiki hii lilichochea wengi kuacha maoni ya kumshauri kutopenda tena mwanasoka.

“Moto sana totoshoo. Ila nakuonya uepukane sana na wanasoka,” mmoja alisema. “Sura nzuri, mwili mzuri na kila kitu kizuri. Usiende tena kwa Neymar sababu sisi ndio tuko!” akarukia shabiki mwingine.

Katika mahojiano yake na jarida la Vogue nchini Brazil, Marquezine alisema: “Yangu na Neymar yalikwisha. Nadhani tulimalizana na kila mtu akafungua sura mpya katika kitabu chake cha maisha.”

“Naomba ieleweke kwamba uamuzi wa sisi kuachana ulikuwa wa Neymar na haukuchochewa na siasa za Brazil. Mjadala huo usirefushwe zaidi ya hapo kwa sababu sipendi sana kuzungumzia maisha yangu binafsi.”