Habari Mseto

Paka na panya baina ya polisi na wachuuzi yavuruga shughuli jijini

July 12th, 2018 1 min read

NA WAANDISHI WETU

SHUGHULI za usafiri na biashara zilivurugwa kwa saa kadhaa katika masoko ya Muthurwa na Wakulima (Marikiti), jijini Nairobi na maeneo yaliyo karibu baada ya wachuuzi kukabiliana na polisi pamoja na askari wa kaunti Alhamisi asubuhi.

Mbunge wa Starehe Charles Njagua alijeruhiwa wakati wa ghasia hizo zilizosababisha msongamano mkubwa wa magari katika barabara za Haile Selassie na Jogoo.

Wachuuzi hao walikuwa wanaandamana kupinga kukamatwa kwa wenzao pamoja na mwenyekiti wao Cyrus Kaguta.

Wafanyabiashara katika masoko hayo vilevile walilalamikia hatua ya serikali ya Kaunti ya Nairobi kubadilisha mfumo wa kulipa ada za kuendesha biashara pamoja na hatua ya askari kutumia nguvu zaidi wakati wanakabiliana na wachuuzi.

Wafanyabiashara hao waliwasha magurudumu na kufunga barabara ya Haile Selassie huku wakirushia waendesha magari mawe.

Hata hivyo, Mkuu wa Operesheni jijini Nairobi Peter Mbaya alikanusha madai ya kudhulumiwa kwa wachuuzi hao akisema waliokamatwa walichochea kupigwa kwa maafisa wa kaunti.

“Sisi si wenda wazimu tupige watu wasio na hatia. Tulikuwa tunakabiliana na wezi waliokimbilia soko la Wakulima kisha mwenyekiti wa wachuuzi akachochea wenzake wawacharaze askari wetu,”alisema Bw Mbaya.

Mkuu wa Polisi Kaunti ya Nairobi Robinson Thuku alithibitisha kukamatwa kwa baadhi ya wachuuzi na kusema sharti wakabiliwe kisheria kabla ya kuachiliwa.

Taharuki ilianza Jumatano wakati askari wa kaunti alipopigwa na wachuuzi hao wakati wa msako wa kuwafurusha wafanyabiashara katika barabara ya Haile Selassie.

Jana, askari wa kaunti waliandamana na polisi waliokuwa na vitoa machozi ili kukabiliana na wachuuzi hao.

Barabara nyingine zilizoathirika katika fujo hizo ni Enterprise, Haile Selassie, Landhies, Ring Road, Wakulima Road, Railway Lane, na River Road.

Bw Njagua ambaye alitibiwa katika hospitali ya Karen na kuruhusiwa kwenda nyumbani aliwashutumu polisi pamoja na askari wa kaunti kwa kutumia nguvu kupita kisiasa wakati wanakabiliana na wachuzi.

Wycliffe Muia, Collins Omullo na Sammy Kimatu