Michezo

Palace yajinasia Ferguson

July 22nd, 2020 1 min read

CHRIS ADUNGO

CRYSTAL Palace wamemsajili beki Nathan Ferguson bila ada yoyote baada ya mkataba wake na kikosi cha West Bromwich Albion katika Ligi ya Daraja ya Kwanza nchini Uingereza (Championship) kutamatika.

Chipukizi huyo wa timu ya Uingereza amerasimisho uhamisho wake hadi Palace kwa mkataba wa miaka mitatu.

Ferguson, 19, alikataa ofay a kurefushwa kwa kandarasi yake kambini mwa Albion waliomsajili akiwa mtoto wa umri wa miaka minane.

“Ferguson ni sajili bora zaidi kwetu. Ni miongoni mwa wanasoka ambao tumekuwa tukiwafuatilia kwa kipindi kirefu na ni afueni kubwa kwamba hatimaye tumejinasia huduma zake,” akasema Mwenyekiti wa Palace, Steve Parish.

Ferguson alikuwa pua na mdomo kuingia katika sajili rasmi ya Palace mnamo Januari 2020 kabla ya uhamisho wake kugonga ukuta kutokana na jeraha la goti.

“Nahisi kwamba kuna mengi mazuri ambayo ninaweza kufanyia kikosi cha Palace. Nimefurahi sana kuingia katika sajili rasmi ya kikosi hiki ambacho nimekuwa pia nikiotea kukichezea,” akasema Ferguson baada ya kutia kidole kwenye mkataba aliopokezwa uwanjani Selhurst Park.