Makala

PAMBO: Tuliza akili unoe makali chumbani

April 4th, 2018 2 min read

Akili inapotulia, mwili huwa unatulia pia na hivyo kuwa katika hali nzuri ya kufurahia maisha ya tendo la ndoa. Kwa watu wengi, tendo hili limekosa ladha kwa sababu hawana muda wao wenyewe. Kutafakari kunaleta ustadi wa kulishana na kufurahia uroda – Zaina Rajab, mtaalamu wa shirika la Hope At Last

Na BENSON MATHEKA

USITUMIE muda wako mwingi kupiga soga ikiwa unataka kuimarisha maisha yako ya uroda. Chukua muda ujitenge na wenzako, utafakari na utaimarisha maisha yako ya burudani.Uchunguzi umebaini kuwa watu wanaotaamuli (meditate) huwa magwiji wa kulishana uroda.

Hasa watafiti walilenga kujua jinsi kutaamuli kunavyohusiana na maisha ya uroda ya wanawake. Waligundua kuwa wanawake wanaotumia muda wao mwingi peke yao wakitafakari kuhusu maisha yao, huwa stadi wa tendo la ndoa na hulifurahia zaidi ya wanaotumia muda wao wakipiga soga.

Watafiti walihoji wanawake 450 walio na umri wa kati ya miaka 17 na 70 kuhusu tajriba yao ya kutaamuli, hisia zao za mapenzi na ikiwa wanafahamu hisia zao za mwili na afya zao.

Wanawake 193 kati ya 450 walikuwa na mazoea ya kutafakari na utafiti uligundua kuwa walikuwa na hamu zaidi ya kufanya mapenzi, weledi wa ngoma yenyewe na uzingativu zaidi wakati wa shughulio.

 

Kufikia kilele cha asali

Kulingana na Profesa Lori A. Brotto, wa chuo kikuu cha British Columbia aliyeshiriki utafiti huo, wanawake wanaotafakari huweza kuchangamkia vyema tendo la ndoa, hulainika vyema na hata kufikia kilele cha tendo la ndoa kuliko wale ambao hawatengi muda wa mazingatio.

“Tuligundua kuwa wanawake wanaojua kutaamuli huwa na hamu ya tendo la ndoa, hisia zao huchangamka haraka. Akili zao huwa tulivu na hufanya maamuzi ya busara jambo ambalo ni muhimu katika uroda,” alieleza mtafiti huyo.

Watafiti wanasema kutaamuli kuna manufaa mengi kwa maisha ya mwanamke ikiwa ni pamoja na kuimarisha akili.

“Akili inapotulia, mwili huwa unatulia pia na hivyo kuwa katika hali nzuri ya kufurahia maisha ya tendo la ndoa. Kwa watu wengi, tendo hili limekosa ladha kwa sababu hawana muda wao wenyewe,” asema Zaina Rajab, mtaalamu wa shirika la Hope At Last.

Anasema kujitenga, kuketi na kutafakari kunasisimua mwili na akili. “Wanasayansi tangu 1995 wamekuwa wakihusisha tabia ya kutafakari na ustadi wa kulishana na kufurahia uroda,” aeleza Bi Zaina.

Kulingana na utafiti wa Profesa Lori, lengo kuu la kutafakari ni kuondoa fikira za wasiwasi hasa ikiwa fikira kama hizi zinamjia mwanamke wakati wa tendo la ndoa.

 

Kutafakari kwa kina

“Tafiti zimeonyesha kuwa kutafakari kwa kina kunaweza kuzuia mawazo kama hayo kuwa sehemu ya akili ya mwanamke na kumfanya achangamkie uroda. Kutafakari kwa kina kunafunza mtu kuleta mawazo yake kwa kile anachotenda,” aeleza Profesa Lori.

Bi Zaina asema kutafakari hufanya mtu kutulia na kuliwazika akilini. Imetambuliwa kuwa wanawake wanaopata shida kuamsha hisia zao za kimapenzi na kutofurahia tendo la ndoa wanaweza kupata matokeo mema wakitafakari.

Na sio wanawake pekee, wanaume wanaweza kuimarisha maisha yao ya uroda ikiwa watakumbatia tabia ya kutaamuli.

“Ikiwa mwanamume ana tatizo la kujikwaa wakati wa tendo la ndoa, dawa ni kutenga muda wa kutafakari. Akizoea kufanya hivi, awe akichukua muda wa kuzama katika tafakuri kwa kina, atapata makali ya kunguruma kwenye shughuli,” asema Bi Zaina.

Profesa Lori ambaye ni mwandishi wa kitabu kiitwacho Better Sex Through Mindfulness kinachoeleza umuhimu wa mazingatio kwa maisha ya tendo la ndoa anasema kutafakari kwa kina kumefanya wanawake wengi waliokosa hisia za mapenzi kubadilika na kuwa magwiji wa ngoma.

Na sio tu kuamsha ladha zao za tendo la ndoa, huwa wanaridhika na kuridhisha wachumba wao,” asema.