HabariMakala

#PandaMitiPendaKenya: Safari ya kupanda miti 1.8 bilioni yang'oa nanga

May 13th, 2018 2 min read

Na WAANDISHI WETU

RAIS Uhuru Kenyatta Jumamosi alizindua kampeni kubwa ya kupanda miti takriban 1.8 bilioni kote nchini katika muda wa miaka mitano ijayo. Waziri wa Mazingira, Keriako Tobiko alisema Serikali inalenga kupanda miti milioni 50 mwaka 2018.

Akihutubu katika shule ya Moi Forces Academy Nairobi, Rais Kenyatta alisema kufikia 2022, Serikali itahakikisha kiwango cha miti nchini ni asilimia 10, kuambatana na viwango vya kimataifa.

“Kiwango cha sasa cha asilimia 7 cha misitu yetu ni cha chini mno na hakiwezi kukidhi mazingira ya taifa linaloendelea kukua kama Kenya. Sharti tupande miti ili turejeshe hadhi ya misitu yetu,”alisema Rais Kenyatta.

Rais aliagiza idara zote za serikali kutumia angalau asilimia 10 ya pesa za huduma kwa jamii kupanda miti katika maeneo mbalimbali nchini.

“Hii si kazi ya mtu mmoja, sharti sisi sote tushirikiane.

“Hali yetu kwa sasa sio tofauti na janga la ukame lililotukumba hivi majuzi. Mazingira yetu ni muhimu zaidi katika maendeleo ya taifa hili kwa sababu kila sekta ya uchumi inategemea mazingira,” aliongeza Rais Kenyatta.

Rais Uhuru Kenyatta, naibu wake William Ruto, Mama wa Taifa Margaret Kenyatta watazama huku Waziri wa Mazingira Keriako Tobiko akipanda mti katika shule ya Moi Forces Academy, Nairobi Mei 12, 2018. Picha/PSCU

Rais alisema kutokana na ukataji wa miti, kiasi cha maji nchini kimepungua na kitaendelea kupungua iwapo hatua madhubuti hazitachukuliwa.

“Ukame umekuwa mkali zaidi ikilinganishwa na hapo awali. Mafuriko yamekuwa jinamizi, lazima tuelewe kwamba majanga tuliyokabiliana nayo yametokana na mabadiliko ya hali ya anga na ni muhimu kutilia maanani suala hilo,” alisema Rais Kenyatta.

Rais alitangaza kuunda Tuzo la Upanzi wa Miti ili kuzawadi watakaopanda na kutunza miti kwa kiwango cha juu nchini.

Naibu Rais William Ruto alisema ifikapo 2022, kila idara ya serikali pamoja na serikali za kaunti zitaonyesha kiwango cha miti zimepanda.

Shughuli hiyo ya upanzi wa miti pia iling’oa nanga katika kaunti kadhaa nchini huku magavana na polisi wa utawala wakiungana na wananchi kupanda miti.

Katika Kaunti ya Machakos, Gavana Dkt Alfred Mutua aliongoza wabunge pamoja na madiwani wa eneo hilo kupanda zaidi ya miche 3,000 katika shule ya msingi ya Makutano DEB.

Wanafunzi wa Moi Forces Academy washirikiana kupanda miti katika shughuli iliyoongozwa na Rais Uhuru Kenyatta Mei 12, 2018. Picha/ PSCU

Wanasiasa wavalia njuga zoezi

Naye Seneta wa Baringo ya Kati Gedion Moi akiandamana na Katibu Mkuu wa chama cha Kanu Nick Salat, Katibu Mkuu wa ODM Edwin Sifuna na mwenzao wa ANC Geoffrey Otsosi waliungana na mbunge wa Samburu Mashariki kupanda miti katika eneo hilo.

Kamishna wa Kaunti ya Makueni, Mohammed Maalim aliongoza maafisa wa kaunti kupanda zaidi ya miche 3,000 karibu na bwawa la Matinga.

Ili kutimiza malengo ya kupanda miti bilioni 1.8, serikali kuu imeshirikiana na mashirika ya yasiyo ya serikali kama vile Nation Media Group.

Naibu Waziri wa Michezo Kassim Farrah (kati) aungana na maafisa wa kulinda misitu katika Shule ya Mzingi ya Ngiine, Meru kupanda miti. Picha/ Gitonga Marete

Kiongozi huyo alisema uhifadhi wa mazingira na upanzi wa miti utachangia katika ajenda ya maendeleo ya serikali.

Wakati wa hotuba yake katika shule ya Moi Forces Academy Nairobi, Rais Kenyatta aliomboleza wananchi waliopoteza maisha yao Nakuru, Tana River na kwingineko na kuahidi kuwa serikali itawasaidia waathiriwa wote wa mafuriko.

“Tutasimama na nyinyi, tutawasaidia mahali mlipo nchini,” alisema kiongozi wa nchi na kuwataka wananchi kuzidi kuonyesha umoja katika kuwasaidia wananchi walioathiriwa.

Alisema Serikali itaendelea kuwaokoa wananchi walioathiriwa na mafuriko na kutoa chakula cha msaada, dawa pamoja na kuwatimizia mahitaji mengine kama vile kutoa maji safi.

Alisema serikali imetenga Sh1.5 bilioni kukabiliana na janga la mafuriko kote nchini na kusisitiza umuhimu mkubwa wa kuhifadhi mazingira.