Pande zote zakubaliana kumsukuma Bashir ICC

Pande zote zakubaliana kumsukuma Bashir ICC

Na MASHIRIKA

KHARTOUM, SUDAN

SUDAN na Mahakama ya Kimataifa kuhusu Uhalifu (ICC), zimetia saini mkataba wa ushirikiano kama hatua moja ya kuanzisha mchakato wa kushtakiwa kwa aliyekuwa rais wa nchi hiyo Omar al-Bashir katika mahakama hiyo kwa kuhusika katika mauaji ya halaiki katika mkoa wa Darfur.

Mwendesha Mashtaka wa ICC, Karim Khan, aliyetaja vita vya Darfur kama kipindi cha giza katika historia ya Sudan, alisema mipango inaendelea ili mahakama hiyo iliyoko The Hague, Uholanzi kufungua ofisi Sudan kukusanya ushahidi zaidi ili kujenga kesi thabiti.

Bashir, 77, amekuwa akitakikana na ICC kwa zaidi ya mwongo mmoja kujibu mashtaka ya mauaji ya halaiki, uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu katika jimbo la Darfur.

Waliokuwa washirika wake wawili pia wanasakwa na ICC kushtakiwa kwa uhalifu wa kivita.

Umoja wa Mataifa unasema kwamba watu 300,000 waliuawa na wengine milioni 2.5 wakafurushwa makwao katika mzozo wa Darfur ambao ulizuka 2003.

Tangu 2019, Sudan imekuwa ikiongozwa na serikali ya mpito ya kijeshi na kiraia ambayo imeapa kuhakikisha waathiriwa wa uhalifu wa kivita chini ya utawala wa Bashir wanapata haki.

Mnamo Alhamisi, Khan aliwaambia wanahabari mjini Khartoum kwamba amefurahi kuripoti kuwa serikali ya mpito imetia saini mkataba wa maelewano na ofisi yake, ambao unajumuisha watu wote ambao kuna vibali vya kuwakamata vilivyotolewa na ICC.

Bashir, aliyetawala Sudan kwa mabavu kwa miongo miwili kabla ya kuondolewa mamlakani kupitia maandamano 2019, amezuiliwa katika gereza la Kober jijini Khartoum.

ICC ilitoa kibali cha kumkamata Bashir 2009 kwa kuhusika na uhalifu wa kivita jimbo la Darfur na baadaye ikaongeza mashtaka ya mauaji ya halaiki dhidi yake.

Bashir amefungwa jela pamoja na maafisa wawili wa vyeo vya juu – aliyekuwa waziri wa Ulinzi, Abdel Rahim Mohamed Hussein na Ahmed Haroun, ambaye alikuwa gavana wa jimbo la South Kordofan.

Mapema wiki hii, baraza la mawaziri la Sudan lilikubaliana kumwasilisha Bashir katika ICC pamoja na waliokuwa maafisa wa serikali yake, uamuzi ambao ni lazima uidhinishwe na baraza kuu la utawala linalojumuisha maafisa wa kijeshi na kiraia.

Lakini Alhamisi, Khan alisema kwamba hatua muhimu zinahitajika kabla ya rais huyo wa zamani kuwasilishwa ICC kufunguliwa mashtaka.

“Kuhamishwa kwa mshukiwa ni hatua muhimu, lakini inafaa kutanguliwa na ushirikiano wa kina,” alisema Khan.

Vita katika mkoa wa Darfur vilianza 2003 wakati waasi wa jamii zisizokuwa za Kiarabu walipoanza mashambulizi wakilalamikia kutengwa na serikali ya Bashir iliyokuwa ya Waarabu wengi.

You can share this post!

Mwashetani aachia Achani tikiti ya ugavana

Wezi wa parachichi wasakwa Kakuzi