Habari Mseto

Panyako awataka wauguzi kutokubali kutishwa bali waendelee na mgomo

December 11th, 2020 1 min read

Na CHARLES WASONGA

CHAMA cha Kitaifa cha Kutetea Masilahi ya Wauguzi (KNUN) kimezishutumu serikali za kaunti kwa kutumia vitisho kama njia ya kuwashinikiza wanachama wake walioajiriwa kwa kandarasi kurejea kazini.

Kwenye taarifa kwa vyombo vya habari Katibu Mkuu wa chama hicho Seth Panyako hata hivyo aliwashauri wahudumu hao wa afya waendelee na mgomo kwa sababu Katiba ya sheria husika za leba zinawapa haki za kufanya hivyo.

“Kile ambacho tunafahamu ni kwamba wafanyakazi wote walioajiri katika mkataba wa kudumu ama kandarasi wako na haki ya kujiunga na vyama vya kutetea masihali ya wafanyakazi na kushiriki migomo endapo watahisi kunyanyaswa na mwajiri wao,” akasema.

Akaongeza Bw Panyako: “Kwa hivyo madai kwamba kuna kandarasi ambayo inawazuia wauguzi walioajiriwa kwa kandarasi kujiunga au kushiriki shughuli za chama chetu hakina mashiko yoyote.”

Haya yanajiri siku ambayo mgomo wa wauguzi umeingia siku yake ya nne ambapo shughuli za matibabu zimesambaratika, wagonjwa wakiteseka kwa kukosa huduma katika hospitali za umma.

Bw Panyako alisema badala ya serikali za kaunti kutoa vitisho wanafaa kuwaita wauguzi hao kwa meza ya mazungumzo ili wajadili namna ya kutimiza matakwa yao

Baraza la Magavana (CoG) kupitia mwenyekiti wake Wycliffe Oparanya limewaomba wahudumu hao wa afya kuelewa hali ngumu inayokabiliwa mataifa yote ulimwenguni kutokana na athari za janga la Covid-19.

“Masuala mengine ambayo wauguzi wameibua yanahusu kaunti husika na yanaweza kutatuliwa kupitia mazungumzo yanayoshirikisha wadau wote. Mgomo sio suluhu kwa changamoto hizi ambazo kimsingi zimesababisha na uhaba wa fedha unaosababishwa na kudorora kwa uchumi,” akasema Gavana huyo wa Kakamega.

Wauguzi katika kaunti mbalimbali nchini walianza mgomo wao Jumatatu wakiitisha marupurupu zaidi, vifaa vya kinga (PPEs), Bima ya Afya, kuajiriwa kwa wauguzi wengine miongoni mwa matakwa mengine.