Kimataifa

Papa adai wanaopinga mashoga wana unafiki

February 8th, 2024 2 min read

NA MASHIRIKA

VATICAN, VATICAN

KIONGOZI wa Kanisa Katoliki duniani Papa Francis amesema anaona “unafiki” katika kauli za watu wanaokosoa uamuzi wake wa kuruhusu makasisi kuwabariki wapenzi wa jinsia moja.

Baraka za LGBT ziliidhinishwa mnamo Januari na hati ya Vatican iitwayo Fiducia Supplicans (Supplicating Trust), lakini hatua hiyo imekumbana na upinzani mkubwa katika Kanisa Katoliki, hasa kutoka kwa maaskofu wa Afrika.

“Hakuna mtu anayekashifiwa ikiwa nitatoa baraka zangu kwa mfanyabiashara ambaye labda anawanyanyasa wateja, na hii ni dhambi kubwa sana. Lakini wananikashifu ikiwa nitawabariki mashogana wasagaji,” Francis aliliambia jarida la Kikatoliki la L’Italia Credere.

“Huu ni unafiki,” alisema.

L’Italia Credere lilitoa vidokezo vya mahojiano hayo Jumatano, siku moja kabla ya kuchapishwa.

Papa Francis pia alisema “daima” anakaribisha makundi ya LGBT na waliooa tena baada ya kutalikiana kwenye sakramenti ya kuungama, kulingana na kifungu kingine kilichochapishwa na vyombo vya habari vya Vatican.

“Hakuna anayepaswa kunyimwa baraka. Kila mtu…kila mtu…kila mtu,” Papa alisema, akirudia kauli mbiu ya maneno matatu aliyotumia mwezi Agosti 2023 wakati wa tamasha la vijana wa Kikatoliki nchini Ureno.

Kiongozi huyo, ambaye alisema kwa ujasiri, “Mimi ni nani nihukumu?” alipoulizwa kuhusu ushoga mwanzoni mwa upapa, ameifanya hoja hiyo kuwa mojawapo ya misheni yake ya kulifanya Kanisa Katoliki liwe karimu zaidi na lisilohukumu.

Wahafidhina wanasema hii inahatarisha kudhoofisha mafundisho ya maadili ya Kanisa.

Ametetea Fiducia Supplicans mara kadhaa, lakini alikiri kupingwa kwake, akisema kwa mfano kwamba mapadre wanapaswa kuzingatia hisia za ndani wakati wa kutoa baraka.

Januari 25, 2024, Papa Francis alisisitiza tena kwamba ushoga si uhalifu, na kwamba tendo lolote la ngono nje ya ndoa ni dhambi, katika jibu la maandishi kwa ombi la ufafanuzi kuhusu matamshi yake wakati wa mahojiano ya hivi karibuni na Shirika moja la Habari la Kimataifa.

Katika mahojiano na shirika hilo, na ambayo yalipeperushwa na kuchapishwa kwa lugha ya Kihispania mnamo Januari 25, 2024, Papa alikuwa amesema kuwa “kuwa ushoga sio kosa. Sio uhalifu.”

Alifafanua kuwa sheria “zisizo za haki” ambazo zinaharamisha ushoga au shughuli za ushoga na kuwahimiza washiriki wa kanisa, pamoja na maaskofu, kuonyesha “huruma” kama Mungu anavyofanya kwa kila mtoto wake.

Katika mahojiano hayo Papa alisema, “Sisi sote ni watoto wa Mungu, na Mungu anatupenda jinsi tulivyo na kwa nguvu ambayo kila mmoja wetu anapigania utu wetu. Kuwa ushoga sio kosa. Sio uhalifu.”