Kimataifa

Papa Francis akatiza likizo kwa sababu ya mafua

March 3rd, 2020 1 min read

MARY WANGARI na MASHIRIKA

PAPA Francis aliyefutilia mbali likizo ya Lenti kwa mara ya kwanza katika hatamu yake kama papa kwa sababu alikuwa anaugua mafua, amepatikana bila virusi vya Corona.

Hii ni kulingana na vyombo vya habari vilivyoripoti hayo mapema Jumanne.

Msemaji wa Vatican Matteo Bruni alisema hakuwa na maoni wakati huo ripoti hiyo ilipotolewa,

Kiongozi huyo wa Kanisa la Katoliki mwenye umri wa miaka 83 aliyetolewa kijisehemu cha pafu lake moja kutokana na maradhi miongo kadhaa iliyopita, pia alifutilia mbali sehemu kubwa ya mikutano wiki iliyopita.

Francis alitarajiwa kushiriki likizo hiyo ya wiki moja na maafisa wakuu wa Vatican iliyoanza Jumapili usiku katika kanisa moja kusini mwa Roma.

Lakini kupitia tangazo lililowapata wengi bila kutarajia saa chache baadaye, alisema atafuatilia shughuli hiyo kutoka chumba chsake cha wageni Vatican.

Ameripotiwa kuugua wakati ambapo taifa la Italia linakabiliana na mkurupuko unaozidi kusambaa wa virusi hatari vya corona.

Idadi ya vifo nchini Italia iliruka hadi 52 kutoka 34 siku iliyotangulia na jumla ya idadi iliyothibitishwa katika taifa lililoathiriwa zaidi barani Uropa ikipita kiwango cha 2,000.