Papa Francis ateua Askofu Anyolo kumrithi Njue

Papa Francis ateua Askofu Anyolo kumrithi Njue

Na BENSON MATHEKA

ASKOFU Mkuu Philip Anyolo wa dayosisi ya Kisumu, ameteuliwa kusimamia dayosisi kuu ya Nairobi ya kanisa Katoliki na kumfanya mrithi wa Kadinali John Njue aliyestaafu mapema mwaka huu.

Uteuzi huo uliofanywa na kiongozi wa Kanisa Katoliki ulimwenguni Papa Francis na kufichuliwa jijini Vatican, Roma Alhamisi, unamfanya Askofu Anyolo kuwa kiongozi wa kanisa hilo nchini Kenya.

Kulingana na Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki nchini (KCCB), habari za uteuzi wa Askofu Anyolo aliyezaliwa Tongaren, Kaunti ya Bungoma, ziliwasilishwa na Mwakilishi wa Papa Francis nchini Askofu Mkuu Hubertus van Megen.

“Ni heshima na furaha yangu kukufahamisha kuwa Papa Francis amemteua Askofu Mkuu Philip Anyolo, ambaye kwa wakati huu anahudumu Kisumu kuwa Askofu Mkuu wa Nairobi,” ilisema barua ya Van Megen kwa KCCB.

Askofu Anyolo amehudumu kama askofu kwa zaidi ya miaka 27 baada ya kutawazwa kasisi Oktoba 15, 1983. Alihudumu kama kasisi kwa miaka 12 hadi Desemba 6, 1995 alipotazwa kuwa askofu wa dayosisi ya Kericho.

Mnamo Mei 23, 2003, alihamishiwa dayosisi ya Homa Bay alikohudumu hadi alipoteuliwa Askofu Mkuu wa dayosisi ya Kisumu mnamo Novemba 15, 2018.Kufuatia uteuzi wake kusimamia dayosisi kuu ya Nairobi, Anyolo atakuwa wa tano kushikilia wadhifa huo.

Watangulizi wake ni Maaskofu John Joseph McCarthy, Kadinali Otunga, Ndingi Mwana Anzeki na John Njue. Tangu Papa Francis alipokubali kustaafu kwa Kadinali John Njue , dayosisi ya Nairobi imekuwa chini ya usimamizi wa Askofu msaidizi David Kamau.

You can share this post!

Shahidi wa kesi dhidi ya Gicheru ICC ‘atoweka’

Kunihusisha na ufisadi kutafeli kwani Wakenya si wajinga- ...

T L