Habari Mseto

Papa Shirandula afariki jijini Nairobi

July 18th, 2020 2 min read

Na WAANDISHI WETU

MWIGIZAJI Papa Shirandula amefariki jijini Nairobi, familia yake imethibitisha Jumamosi.

Ina maana janga la corona limepokonya taifa la Kenya shujaa kutoka kwa tasnia ya uigizaji na burudani.

Jina halisi la staa huyo wa uigizaji na pia chale maarufu – mchekeshaji – ni Charles Bukeko na amefariki asubuhi akiwa na umri wa miaka 58.

Shemeji yake, Bw Ronald Wanyama amesema Papa, anavyofahamika kwa wengi, alipata matatizo ya kupumua ndipo akapelekwa hadi Hospitali ya Karen.

“Inahuzunisha hakuondoka hospitalini akiwa hai. Alikuwa amepatikana kuugua Covid-19. Tunahuzunika sana,” amesema.

Bw Wanyama amesema marehemu alikuwa amesafiri hadi eneo la Magharibi akarudi Nairobi Jumapili iliyopita, ndipo akaanza kuugua.

Bukeko alikuwa mwigizaji mkuu katika kipindi cha ucheshi cha ‘Papa Shirandula’ ambacho hupeperushwa katika runinga ya Citizen, ambacho alikitunga mwenyewe.

Alipata umaarufu kimataifa pia kupitia tangazo la kibiashara la Coca-Cola lililoonyeshwa kote ulimwenguni miaka ya tisini.

Rais Uhuru Kenyatta ameongoza Wakenya wengine wa tabaka mbalimbali kutuma salamu za pole kwa familia ya marehemu.

Katika ujumbe wake, Rais amemsifu marehemu kwa kuchangia katika ukuzaji wa sekta ya burudani.

Bukeko alianza uigizaji katika ukumbi wa Kenya National Theatre mapema miaka ya tisini na mwaka wa 2010 alishinda tuzo ya mwigizaji bora wa vipindi vya runinga.

Ameacha mjane Beatrice Ebbie Andega na watoto watatu Tony, Charlie na Wendy.

Hivi majuzi, alishirikishwa katika video ya wimbo ‘Nakulove’ wa msanii wa nyimbo za kufoka Kennedy Ombima almaarufu kama King Kaka akishirikiana na Paskal Tokodi.

“Ukatili wa kifo umetupokonya msanii shupavu ambaye vichekesho vyake havikufurahisha tu bali pia vilielimisha vizazi vingi,” amesema Gavana wa Kakamega, Bw Wycliffe Oparanya.

Wasanii wengi wamemsifu kama mtu ambaye alijitolea kukuza wale chipukizi bila ubaguzi.

Katika mahojiano ya awali wakati wa uhai wake, Papa Shirandula alikuwa amesema azimio lake lilikuwa ni kuona sekta ya uigizaji ikitoa nafasi za ajira kwa wasanii.

Alieleza kuwa, wasanii wanapaswa kukumbuka wakati wote kwamba kazi yao inafaa kuzingatia zaidi mchango utakaoleta katika jamii.

“Inafaa wakumbuke kila wakati kuwa jambo muhimu katika maisha sio tu kuhusu pesa ulizo nazo bali pia tofauti unayoleta kwa maisha ya mtu. Mimi huhisi vizuri sana wakati tunakuza talanta, na kipindi chetu (Papa Shirandula) huajiri watu zaidi ya 1,500,” alisema katika mahojiano hayo yaliyochapishwa kwa gazeti la Daily Nation.

 

Waandishi ni Benson Matheka, Justus Wanga na Valentine Obara