Habari za Kitaifa

Pasaka: Askofu Martin Kivuva ataka serikali kuteremsha gharama ya maisha

March 29th, 2024 2 min read

NA JURGEN NAMBEKA

WAKRISTO walianza kuadhimisha sherehe za Pasaka kwa kushiriki Njia ya Msalaba mnamo Ijumaa ambapo viongozi wa kidini waliomba Rais William Ruto kutatua matatizo mbalimbali yanayokumba nchi.

Askofu wa dayosisi ya Mombasa Martin Kivuva ambaye pia anahudumu kama Mwenyekiti wa Kongamano la Maaskofu wa kikatoliki nchini Kenya (CCBK) ameitaka serikali ya Kenya Kwanza kutatua shida mbalimbali zinazowakumbwa Wakenya kama njia ya kuwazuia kuondoka nchini.

Akizungumza jijini Mombasa wakati wa ibada ya Njia ya Msalaba, Askofu Kivuva, alieleza kuwa gharama ya juu ya maisha, ushuru wa juu, na ukosefu wa nafasi za ajira vimechangia pakubwa kwa Wakenya kuhamia nchi za ughaibuni.

Ijumaa Njema huadhimishwa kuashiria Ijumaa ya mwisho ambayo Yesu Kristo alipitia mateso mengi, na kusulibiwa–kwa mujibu wa Wakristo–na kufa na kisha kuzikwa. Siku hii huadhimishwa na wakristo wengi ulimwenguni. Ni kama kukumbuka ya mateso ya Yesu Kristo kila mwaka baada ya mfungo wa siku 40.

“Tunapitia matatizo mengi kama tu yale ambayo Yesu alipitia. Haya matatizo ni ya kifedha, ya kiafya na hata saa nyingine ya kiuongozi Tunamwomba Mungu atusaidia kuepuka. Masuala mengi yanawakumba Wakenya,” akasema Askofu Kivuva.

Kulingana naye, shida zinazoikumba nchi, kama vile mgomo wa madaktari na pande husika kukosa kupata suluhu, zinafanya Wakenya wengi kutaabika.

“Masuala ni mengi sana, sio mshahara duni huku Wakenya wakiwa na majukumu mengi. Ni muhimu sana kwa Rais William Ruto na mawaziri wake na hata viongozi wengine kufanya juhudi kushughulikia shida hizi. Matatizo haya yanapaswa kutatuliwa ili wakenya waishi vyema,’ akasema.

Askofu huyo pia aliwaomba Wakenya wawajibike na kujitenga na sifa mbaya ya ufisadi ambayo imewaharibia jina.

Alieleza kuwa Wakenya wanapaswa kuepuka majaribu ya kutarajia kupata mali na fedha bila wao kutia bidii kazini.

“Wakenya ni watu wenye bidii. Tunafaa kuungana na kukabiliana na zimwi hili la ufisadi ili nchi yetu iwe nzuri,” akashauri.

Kwingeneko, Mamlaka ya Masuala ya Ubaharia (KMA), imeeleza kuwa imeweka mikakati kabambe ya kuwalinda Wakenya wanaposherehekea msimu wa Pasaka katika sehemu mbalimbali za nchi zenye maziwa na bahari.

Akizungumza baada ya kuzindua mkakati wa kulinda ufuo wa umma wa Jomo Kenyatta almaarufu Pirates Beach, Mkurugenzi Mkuu wa KMA Mhandisi Martin Dzombo Munga alieleza kuwa taasisi za kiusalama zilikuwa zimejitolea kuhakikisha kuwa hakuna Mkenya ambaye atapoteza maisha baharini.

“Ningependa kuwatangazia kuwa tangu Desemba 2023 hatujapata ajali hata moja ya mtu kuzama baharini. Hili ni jambo zuri ila leo tumejitoekza hapa kuhakikisha kuwa, tukiripoti kutokuwa na ajali isiwe ni bahati, bali kwa sababu ya mikakati kabambe iliyowekwa kuwalindaa Wakenya,”akasema Bw Munga.

Kwa mujibu wake, KMA pamoja na polisi walikuwa wamewahusisha hata makundi ya kusimamia fukwe(BMU) kuwasaidia kuangalia shughuli zinavyoendelea baharini na hata kushughulikia dharura zote zitakazotokea.

Waliwataka Wakenya wanaozuru sehemu hiyo kujivinjari kuwa majini wakati ambapo kuna mwangaza na kutoka pindi tu giza linapoanza kuingia. Alihoji kuwa hili lingewasaidia kuona na kushughulikia dharura yoyote inayotokea.

Mamlaka hiyo ilikuwa pia imesisitiza kuwa, yeyote atakayekumbwa na shida yote ufuoni apige ripoti katika kituo cha polisi ili kusaidia kushughulikia kesi za siku za usoni.