Makala

Pasaka yakutana na Ramadhani Pwani

March 21st, 2024 2 min read

NA ANTHONY KITIMO

WAKRISTU wiki ijayo wanasherekea sikukuu ya Pasaka, wakati ambao wengi hupenda kusafiri hadi Kaunti ya Mombasa kusherekea na familia zao.

Lakini mwaka huu 2024, kwa wale wanaopenda mapochopocho wakati wa mchana, hawana budi ila kusubiri hadi jioni kwani mikahawa mingi maarufu itakuwa imefungwa, ikizingatiwa ni msimu wa mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani wenye hadhi kubwa sana katika kalenda ya Kiislamu.

Wanaopenda vyakula mbalimbali vya kipwani kama biriyani, pilau, na mandi katika mikahawa kama vile Barka, Tarboush, Cafe Point, na Mombasa Dishes, itabidi wasubiri hadi Waislamu wafungue kwani wanaomiliki mikahawa hiyo ni Waislamu.

Ingawa hivyo, wamiliki wa mikahawa hiyo wamesema wako tayari kupokea wageni na wamejipanga kuwafurahisha kama kawaida baada ya futari.

Ni dhahiri kipindi hiki cha mfungo wa Ramadhani kitakuwa na mabadiliko mengi huku Wakiristu wengi wakisherekea Pasaka.

Wakati wa mfungo wa Ramadhani, mja Mwislamu anahitajika kujizuia kunywa na kula kutoka alfajiri–kuchomoza kwa jua–mpaka maghrib jua linapozama.

Hata hivyo, wanaopenda mapochopocho yaliyopikwa kisawasawa wanasema hawana budi ila kusubiri hadi jioni kwani ni nadra sana kushiriki sherehe za Pasaka na familia.

“Ninatarajia wageni kutoka Nyeri na hupenda wali wa biriyani hivyo basi tutangoja hadi mkahawa wa Tarboush ufunguliwe jioni ndipo tukajivinjari,” alisema Bw John Mwangi, mkazi wa Mombasa.

Katika mikahawa hiyo maarufu, wamiliki tangu mfungo uanze, wamewafahamisha wateja wao kuhusu mabadiliko hayo ya ratiba ambapo wanafungua mikahawa jioni kuanza kwa futari na kuendelea.

“Tumewaeleza wateja wetu katika mitandao yetu ya kijamii kuwa tutakuwa na mabadiliko na kwamba tumefunga kuanzia asubuhi hadi jioni ndipo hata wale wageni wanaokuja kutoka maeneo mengine wasitaabike,” akasema Abdhulmalik Ahmad, meneja wa hoteli ya Cafe Point.

Baadhi ya hoteli kama Barka sasa zinafunguliwa kuanzia saa kumi jioni ambapo wateja wanapaswa kununua chakula na kuondoka.

“Haturuhusu mtu kula hotelini wakati huo hadi saa kumi na mbili jioni watu wanapofungua saumu ndipo wanaweza kuja na kula wakiwa wameketi,” alisema Bw Said Nur, meneja wa hoteli ya Barka.

Wakati wa sherehe mbalimbali, Kaunti ya Mombasa na nyingine za Pwani, hupata wageni chungu nzima lakini mwaka huu 2024 wakati wa Pasaka, wamiliki wa hoteli wanahofia idadi hiyo huenda ikapungua kufuatia kalenda mpya ya masomo ambapo shule nyingi zinatarajiwa kufungwa siku moja kabla sikukuu hiyo.

Bw Sam Ikwaye, mkuu wa chama cha wamiliki wa hoteli Mombasa, alisema kwa sasa hoteli nyingi hazijapata wageni na ziko na wageni takribani asilimia 60.

“Ni vigumu familia kusafiri siku moja tu badda ya shule kufungwa… ndio maana tuko na wageni wachache pia ikizingatiwa Waislamu wengi wako kwa mfungo,” alisema Bw Ikwaye.