Habari Mseto

Pasta afumaniwa na polisi akifukua miili ili auze shamba

May 23rd, 2019 1 min read

Na PETER MBURU

POLISI eneo la Naivasha, Kaunti ya Nakuru Alhamisi walimkamata mhubiri, baada ya kumfumania akifukua miili ya watu wa familia yake, ili auze shamba.

Samuel Macharia, mhubiri kutoka Nairobi alikamatwa nyumbani kwake katika kijiji cha Kinamba, akiwa tayari amefukua miili ya watu watatu; wa mamake, mkewe wa kwanza na mwanawe wa kiume.

Alikuwa akitaka kufukua makaburi saba katika shamba hilo, ili aliuze kwa mtu anayefanya kazi ya kuchimba timbo.

Alisema kuwa alikuwa akipanga kuzika maiti hizo zilizozikwa kati ya 1975 na 2016 tena, katika shamba lingine baada ya kuuza hilo.

Hata hivyo, alikamatwa kwa kuwa hakuifukua akifuata sheria, akijitetea kuwa gharama za kufukua miili akipitia njia ya korti ni ghali mno.

“Nilikuwa nimependekeza kuuza sehemu nyingine ya shamba lakini mnunuzi aliposema anataka hapo sikuweza kupata pesa za kufukua maiti hizo. Gharama ya kufukua mwili wa mtu mzima ni Sh50,000 na wa mtoto ni Sh30,000 nikipitia kortini na niliona zingezipata,” akasema mwanamume huyo.

Majirani, hata hivyo, walisema hali ya watu kufukua miili eneo hilo imekuwa kawaida, wakisema watu mara kwa mara wamelazimika kufanya hivyo kwa sababu tofauti.