Dondoo

Pasta ajuta kuvuruga wapenzi

October 15th, 2019 1 min read

Na LEAH MAKENA

KUU, CHUKA

PASTA wa hapa alijitosa kwenye balaa alipoingilia uhusiano wa wapenzi waliokuwa marafiki zake wa dhati kwa kushawishi jamaa kutema demu akidai angemrudisha nyuma.

Mtumishi huyu alimtaka jamaa kuwa akiandamana naye katika safari zake za kuhubiri.

Jamaa alikuwa miongoni mwa vijana waliojitolea kanisani na demu alikuwa akimkosoa kwa kutozingatia maisha yake binafsi kwa vile hakuwa akilipwa na pasta.

Kulingana na kidosho, jamaa alikuwa ameanza kuparara na kuishi maisha ya ufukara kwa kukosa pesa za kujikimu kwa sababu hakuwa akilipwa kwa kazi aliyofanya kanisani.

Demu alipoanza kumpa presha, jamaa alieleza pasta ambaye alimtaka ateme kidosho huyo.

Pasta alidai kuwa kidosho huyo hakuwa na nia njema na polo kwa kujaribu kumuondoa kwenye huduma kanisani.

Inasemekana pasta alimpigia simu kidosho na kumtaka kutafuta mume atakayempa pesa baada ya kufanya kazi.

Huo ndio ulikuwa mwisho wa uhusiano wa polo na kipusa huyo kwani jamaa alikatiza mazungumzo na kuanza uhusiano mpya na dada aliyekuwa pia akihudumu kanisani bila kulipwa.

Kidosho alikerwa na habari hizo na akamvamia pasta kwenye ofisi yake na kumfokea vikali kwa kuingilia uhusiano wake na jamaa.

“Unajua mangapi ya wanandoa na haujaoa? Kazi ni kupumbaza vijana wa watu wasifanye kazi ilhali wewe unapata mshahara kila baada ya mwezi. Utasalia na laana kila uchao kwa kuvuruga maisha ya watu na iwapo hutakoma utajuta,” kidosho aliwaka.

Kwa muda wote kidosho aliokuwa akiwaka kwa hasira, pasta alisalia kimya akihofia kipusa angemtwanga.

Hata hivyo, licha ya hasira za kipusa hakubadilisha msimamo wake na kusisitiza hakustahili kuwa mke wa jamaa.