Dondoo

Pasta akataa harusi ya mpenzi wa zamani

April 29th, 2019 1 min read

Na Ludovick Mbogholi
MOMBASA MJINI

Kisanga kilizuka mjini hapa pasta alipokataa kuunganisha wachumba kuwa mume na mke dakika za mwisho siku ya harusi.

Maharusi walifika kanisani kufunga pingu za maisha lakini mtu wa Mungu akakataa. Baadaye ilibainika kwamba bi harusi alikuwa mchumba wake kabla ya kumuacha na kumchumbia bw harusi.

Kulingana na mdokezi, ilikuwa imewachukua wachumba muda mrefu kupanga harusi na siku ilipofika waliwasili kanisani wakiandamana na wapambe wao wakitaka kufungishwa ndoa.

“Siwezi kufanya hivyo, tafuteni mchungaji mwingine,” pasta aliwaambia maharusi hao.

Wapambe walitaka kuelezwa sababu za mchungaji kukataa kutimiza agano lake na maharusi na wakashtushwa na jibu lake.

“Maharusi hawa hawaaminiani, ndoa yao huenda isidumu, nitakuwa nafanya kazi asiyoipenda Mungu, kwanza lazima wajitakase wasafiane nia. Pili siwezi kumkufuru Mungu kwa kufungisha ndoa ambayo haitakuwa na uaminifu,” alidai mchungaji.

Mmoja wa wapambe wa bi harusi alifahamu kiini na akatoboa siri.

“Bi harusi awali alikuwa mpenzi wa pasta, lakini walitofautiana akampata huyu anayetaka kufunga naye pingu za maisha,” mpambe alitoboa siri.

Mchungaji kusikia hivyo alifoka.

“Sifungishi ndoa ya mwanamke asiyekuwa mwaminifu, nimepata maono kutoka kwa Mungu kuwa, huyu hawezi kuishi na mwanamume kutokana na ukosefu wa utulivu,” alidai mchungaji. Maneno yake yalimchemsha bi harusi akamkemea vikali.

“Wewe hufai kuhudumia kondoo, una tabia mbovu na hustahili kuitwa mtu wa Mungu, ushindwe katika jina la Yesu,” bi. Harusi aliwaka kwa hasira akimkemea mchungaji.

Ilibidi maharusi waondoke pasta alipokaa ngumu.

“Kumbe wewe ni mchungaji usiyetaka kupitwa na marinda… tamaa yako ya fisi itakuuwa uzikwe na wanawake uliowachezea, ukawatumia na kuwatupa,” alifoka mpambe mmoja wa bw harusi.