Kimataifa

Pasta auawa na mamba akibatiza waumini ziwani

June 7th, 2018 1 min read

Na MASHIRIKA

MERKEB TABYA, ETHIOPIA

PASTA wa kanisa la Kiprotestanti aliuawa na mamba alipokuwa akibatiza waumini karibu na ziwa lililo kusini mwa Ethiopia.

Kulingana na mashirika ya habari, Docho Eshete alikuwa akibatiza waumini karibu 80 wa kanisa lake Jumapili asubuhi katika Ziwa Abaya lililo mjini Arba Minch, Wilaya ya Merkeb Tabya.

Shirika la habari la BBC lilinukuu wakazi wakisema kwamba mamba huyo aliruka ghafla kutoka majini wakati wa ubatizo na kumshambulia mhubiri na kumsababishia majeraha mabaya miguuni, mgongoni na mkononi akafariki.

“Alibatiza mtu wa kwanza kisha akaelekea kubatiza mwingine lakini ghafla, mamba aliruka kutoka kwa ziwa akamnyakua pasta,” BBC ilimnukuu mkazi wa eneo hilo Ketema Kairo.

Wavuvi na wakazi walijitahidi kumwokoa lakini hawakufanikiwa, ikabidi watumie neti za kuvua samaki kumzuia mamba kutoroka na mwili wake, kwa mujibu wa afisa wa polisi Euwnetu Kanko.