Dondoo

Pasta amfurusha mke kwa kutisha kusambaratisha kanisa

May 9th, 2018 1 min read

Na CORNELIUS MUTISYA

NZAIKONI, MACHAKOS

PASTA wa kanisa moja eneo hili alimfurusha mkewe akidai alikuwa amechoshwa na tabia yake ya udaku. Jamaa alisema tabia ya mkewe nusura isambaratishe kanisa lake na hangemvumilia.

Kulingana na mdokezi, pasta alifungua kanisa hapa na likavutia watu wengi. Waumini walikuwa wakifurika kanisani kupata chakula halisi cha roho.

Inasemekana kwamba mkewe alipewa jukumu la kuwapa ushauri nasaha wanawake kanisani.

Hata hivyo, wanawake hao hawakuwa na imani na uongozi wake wakidai alikuwa mwenye kiburi na mjeuri kupindukia.

Yasemekana alikuwa akiwasengenya akina mama hao kokote alikoenda.

Hata akiwa saluni, ama akinunua mboga sokoni, alikuwa akieneza porojo kuhusu vile wanawake wa kanisa la mumewe walikuwa wachoyo, washamba na waliokosa hadhi ya kuitwa wanawake kwa sababu ya kutojua kujipodoa.

Kulingana na mdokezi, wanawake hao walipochoshwa na udaku mke wa pasta, walianza kususia ibada.

Hata hivyo, mmoja wao aliwashauri wamjulishe pasta wao kabla ya kuchukua hatua yoyote.

“Akina mama hao walimwendea Mtumishi wa Mungu ofisini na wakamueleza malalamishi yao. Pasta aliwaomba radhi na akawaahidi kuchukua hatua muafaka,’’ akasema mpambe wetu.

Duru zaarifu kuwa, pasta alifululiza hadi nyumbani na kumuamuru mkewe kufunganya virago vyake na kutokomea kwa kumharibia sifa.

“Siwezi nikakubali kanisa langu lisambaratike kwa sababu ya sususu na umbea wako. Nenda zako. Wewe ni bure kabisa!’’ pasta alimfokea mkewe.

Twaarifiwa kwamba, mke wa pasta alifunganya virago vyake na kutokomea kusikojulikana. Aliacha nyuma watoto wawili ambao wanaendelea kutunzwa na baba yao huku kanisa likizidi kushamiri.

…WAZO BONZO…