Kimataifa

Pasta ampiga risasi na kumuua mvamizi mwenye bunduki

June 20th, 2018 1 min read

Na MASHIRIKA

WASHINGTON, AMERIKA

PASTA alimpiga risasi na kumuua mvamizi aliyeshambulia duka la jumla la Walmart.

Ripoti zilisema mshambuliaji aliyetambuliwa kama Tim Day mwenye umri wa miaka 44 alishambulia duka hilo mashuhuri na kufyatua risasi zilizojeruhi watu wawili.

Ilisemekana pia mvamizi huyo alijaribu kuiba magari sita kwa kulazimisha waendeshaji waondoke akitishia kuwapiga risasi.

Pasta mwenye umri wa miaka 47 ambaye anamiliki bunduki kihalali aliingilia kati na kufanikiwa kumuua Day kabla asababishe hasara zaidi.

Kulingana na mashirika ya habari, pasta huyo ambaye aliomba aitambuliwe pia ni afisa wa zimamoto wa kujitolea na ni daktari.

“Bila yeye watu wangapi wangeuawa?” akauliza mmoja wa waathiriwa aliyepigwa risasi mkononi alipokataa kusimamisha gari lake.

Polisi walinukuliwa kusema kuwa waliitwa mwendo was aa kumi na moja jioni kuhusu jamaa aliyekuwa akijaribu kuteka watu nyara kwenye magari yao.

Walisema Day alifika katika duka hilo la jumla dakika 30 baadaye baada ya kushindwa kuiba gari akaanza kufyatua risasi kiholela.

Pasta alimpiga risasi alipokuwa akijaribu kumwibia mtu mwingine gari lake. Baada ya kumpiga risasi, pasta huyo alichukua vifaa vyake vya matibabu akampa huduma ya kwanza kabla madaktari kuwasili.

Ripoti zinasema mshambuliaji alikuwa mraibu wa dawa za kulevya aliyekumbwa pia na matatizo ya kiakili.

-Imekusanywa na Valentine Obara