Dondoo

Pasta anaswa na mkewe kona mbaya

June 28th, 2020 1 min read

Na NICHOLAS CHERUIYOT

AINAMOI, Kericho

KULIZUKA kioja eneo hili polo na mkewe walipolumbana vikali kisha wakapiga magoti kuombeana.

Duru zetu zaarifu kuwa polo hudai ni mwinjilisti na juzi alitoka nyumbani baada ya kumwambia mkewe anaenda kuhubiri eneo la mbali.

Mkewe akamsindikiza na kumtakia kila la heri, lakini baadaye akapata fununu kuwa mumewe alienda kushiriki uasherati na kimada wake anayeishi mji wa mbali.

Siku ya kisanga, polo alirudi nyumbani akiwa na Biblia mkononi huku akiimba wimbo wa dini.

“Nina furaha kuwapata mkiwa salama. Nilifanikiwa kuhubiri injili na watu kadhaa waliokoka,” jamaa akamwambia mkewe.

Hata hivyo, mkewe alilipuka kwa hasira akimlaumu jamaa kwa uasherati.

“Acha huo ukora wako! Nimepata habari kamili ulitumia nafasi hiyo kunisaliti na hawara wako. Rudi utokako!” Mkewe aliwaka kwa hamaki.

Jamaa alishtuka kujua chuma chake ki motoni na akaloa jasho akiwa amekabiliwa na kikohozi.

“Fitina ulizopata zatokana na matendo ya shetani mwenyewe. Achana na hayo na unipe makaribisho ninayostahili,” jamaa alisema.

Hapo ndipo sokomoko ilishika kasi kwani mkewe aliacha kunung’unika kwa sauti ya kawaida na akawika kwa hasira.

Jombi alijua alikuwa amesukumwa kona mbaya na akaamua kupiga magoti kwenye matope na kutoa maombi ya kipekee.

“Naomba mke wangu aone mwanga na asipotoshwe na shetani ili aniache niendeleze huduma,” jamaa alisali na hasira za kipusa zikapoa ghafla.

“Naye mama watoto alipiga magoti pia na kuomba kuwa Mungu akomeshe tamaa ya ufuska uliomteka mumewe,” mdaku akaeleza.

Kisha mke alisema amemsamehe mumewe ambaye naye aliahidi kuwa mwaminifu kwake.