Dondoo

Pasta aonya mwanawe asipotoshe vidosho kanisani

January 30th, 2019 1 min read

Na JOHN MUSYOKI

Machakos Mjini

KULIZUKA kioja mtaani hapa pasta alipomkemea mwanawe akimlaumu kwa kutaka kupotosha kipusa muumini wa kanisa lake.? Inasemekana kijana wa pasta alikuwa akimmezea mate kichuna wa kanisa hilo japo hakuwa akienda kanisani.

Siku ya kioja, jamaa alijipata pabaya babake alipompata akipiga gumzo na mwanadada huyo na akamkemea mbele ya umati wa watu.

“Unataka nini hapa kanisani.Kwanza wewe huwa haushiriki katika kanisa hili. Unafanya nini na dada huyu.Wewe ni mwanangu lakini sitakubali upotoshe msichana huyu.Tabia yako haifai. Nimekuonya mara nyingi uokoke lakini umekuwa na roho ya chuma,” pasta alimwambia mwanawe.

Yasemekana jamaa hakuruhusu baba yake aendelee kumdhalilisha mbele ya watu. Alimwambia baba yake hakufaa kuingilia maisha yake ya kibinafsi.

“Wewe ni pasta na baba yangu hilo sikatai. Lakini kinachokuwasha ni nini. Hata kama sijaokoka hufai kunizuia kumchumbia mwanadada huyu. Hautanizuia kufanya jinsi ninavyotaka,” polo alimwambia babake.

Pasta alikaa ngumu na kumwamuru jamaa kuondoka uwanja wa kanisa.

“Kufumba na kufumbua sitaki kukuona ukisimama na mwanadada huyu na ukiendelea kunikaidi nitakuonyesha cha mtema kuni,” pasta alitisha.

Hali ilizidi kuchacha ikawa ni vuta nikuvute kila mmoja akitetea upande wake.

“Kwa sasa ningependa ujue kwamba nampenda mwanadada huyu kwa dhati.Naondoka sasa hivi lakini ningependa kukuhakikishia kwamba hautanuzuia,” jamaa aliongeza na kuondoka.

Inasemekana mwanadada hakusema lolote mtu na baba yake walipokuwa wakilaumiana kwa sababu yake.? Umati ulianza kunong’onezana kuhusu kisa hicho huku wengi wakipigwa na butwaa na kukosa majibu ya maswali waliyojiuliza.

Hata hivyo, haikujulikana kilichojiri baada ya kioja hicho.