Makala

Pasta asema tendo la ndoa ndio ‘mambo yote’

March 16th, 2024 2 min read

NA WANDERI KAMAU

KWA kawaida, mapasta na wahubiri huwa wanatarajiwa kuhubiri mafundisho ya kukuza Imani za kiroho za washirika wao, kazi ambayo wengi hufanya kwa uadilifu ili kumfurahisha Mungu.

Kwa kutekeleza kazi hiyo, wapo wahubiri wanaoona aibu kuzungumzia suala muhimu katika ndoa–mume na mke kuonana kimwili kwa njia iliyohalalishwa.

Pasta Sue Munene amejitokeza waziwazi na kujitwika jukumu la kuwahubiria washirika wake “injili ya masuala ya ngono”, akishikilia kuwa suala hilo ndilo kiini cha talaka nyingi ambazo zimekuwa zikishuhudiwa miongoni mwa wanandoa.

Pasta Sue Munene akihubiri. PICHA | MAKTABA

Kwenye mahojiano ya kipekee na Taifa Leo, Pasta Munene alisema kuwa ingawa huwa anahubiri masuala ya injili “mafundisho kuhusu ngono ndio hujumuisha asilimia kubwa ya mahubiri anayotoa”.

“Ukweli ni kuwa, matatizo mengi yanayowakumba wanandoa yanatokana na masuala ya ngono. Hata hivyo, wanandoa wengi huwa hawataki kujitokeza hadharani kueleza matatizo ambayo huwa yanawakumba. Ndipo nimeamua kujitwika jukumu la kutoa mafunzo kwa wanandoa kuhusu ngono bila kumwogopa mtu yeyote,” akasema Pasta Munene, anayeongoza kanisa lake la Overcomers Hope Ministries, lililo eneo la Kasarani, Kaunti ya Nairobi.

Pasta Munene ni mke wa Pasta Joseph Munene, na wamekuwa kwenye ndoa kwa zaidi ya miaka 20.

Hata hivyo, anasema kuwa mafundisho yake huwalenga wanandoa, kwani tendo la ngono linafaa kufanywa na watu waliooana pekee.

“Ingawa huwa ninatoa mafunzo kuhusu ngono, hilo halimaanishi khuwa ninawarai watu kushiriki ngono ovyo, bila kuwajibika. Kwanza, msimamo wangu ni kuwa watu ambao hawajaoana hawafai kushiriki ngono, kwani ni jambo linalozuiwa na mafundisho ya kidini,” akasema.

Anaeleza aliamua kujitwika mzigo wa kutoa mafunzo kuhusu ngono, kwani watu wengi huwa wanaogopa kuzungumzia masuala hayo, licha ya umuhimu wake.

“Msingi wa ndoa nzuri na thabiti ni tendo la ngono. Tendo hilo ndilo huwa linatumika na wanandoa kusuluhisha matatizo ama tofauti zinazoibuka baina yao, kwani linafaa kuwa chemichemi ya furaha. Hata hivyo, kuna matatizo mengi yanayoikumba ndoa husika, ikiwa wanandoa hawaridhishani. Hapo ndipo huwa unasikia wanandoa wakiwa na mahusiano ya nje ili kujiridhisha,” akasema.

Mhubiri huyo anasema hajutii uamuzi aliochukua, kwani amewasaidia wanandoa wengi, hasa kupitia warsha tofauti za mafunzo ya mume na mke kuonana kimwili.

Pasta Sue Munene akitoa mafundisho muhimu ya nguzo za ndoa, likiwemo suala la wanandoa kuonana kimwili. PICHA | MAKTABA

Warsha hizo amekuwa akiandaa katika sehemu tofauti nchini.

“Huwa pia ninawafunza vijana walio karibu kuingia kwenye ndoa kuhusu masuala tofauti ya ngono, hasa wakati huu ambapo kuna maradhi hatari yanayohusiana na ngono kama vile Ukimwi, Kisonono, Kaswende kati ya mengine mengi,” akasema.

Anasema haogopi lolote na kwamba ataendelea kutoa mafunzo hayo ili “kukiokoa kizazi cha sasa dhidi ya hatari inazokikabili”.

Ikiwa wanandoa wote wawili wako sawa kiafya na wamejitayarisha kisaikolojia na kihisia, mhubiri huyo anasema hakuna mipaka kuhusu ni mara ngapi wanandoa wanafaa kushiriki tendo la ndoa kwa wiki moja, japo anaeleza kuwa panafaa pawepo na maelewano baina ya wanandoa.

“Inaweza kuwa mara tatu, mara nne au hata mara tano. Tendo hilo linafaa kufanywa wakati kila mwanandoa anahisi hitaji lake na wakati wote wanahitaji kutimiza haja zao za kimapenzi. Huo ndio wakati huwa linapendeza zaidi,” akasema.