Habari za Kitaifa

Pasta ashtakiwa kula Sh2.6m za muumini kwa dili ya ng’ombe

March 5th, 2024 2 min read

NA RICHARD MUNGUTI

MHUBIRI ameshtakiwa kwa kumlaghai mshirika wake zaidi ya Sh2.6 milioni alizodai angeziwekeza katika biashara ya ufugaji wa zaidi ya ng’ombe 100 katika Kaunti ya Narok.

Pasta Johnson Kintalel Nkuku alikana shtaka la kumlaghai Yvonne Teeti pesa hizo aliposhtakiwa mbele ya hakimu mwandamizi Robinson Ondieki katika Mahakama ya Milimani, Nairobi.

Baada ya kukana shtaka Bi Teeti alijitosa kizimbani kueleza mahakama jinsi alivyotapeliwa na “Baba wangu kiroho na Mtu wa Mungu.”

Akihojiwa na kiongozi wa mashtaka kueleza mahakama ikiwa alikuwa anamfahamu mshtakiwa Bi Teeti alisema “nilimfahamu Bw Nkuku kwa zaidi ya miaka saba kabla ya kisa hiki.”

Muumini huyo alikiri alikuwa akihudhuria ibada ya kila Jumapili katika Kanisa la Dominion Church lililoko Kaunti ya Narok, na “ilinilazimu kutii sauti ya Mungu kupitia kwa mtumishi wake.”

“Singekaidi sauti ya Mungu kupitia kwa mtumishi wake Bw Nkuku kuwa niwekeze katika ufugaji wa mifugo,” alisema mlalamishi huyo.

Mlalamishi huyo alisema Bw Nkuku aliahidi kutunza ng’ombe hao katika shamba lake.

Hakimu alielezwa mlalamishi na Pasta Nkuku walikubaliana kwamba “atakuwa anatuma pesa za kununua mifugo hao na kuwatunza kwa vile alikuwa amesheheni katika kazi ya kulisha mifugo na kuwatunza.”

Mahakama ilielezwa mlalamishi alikuwa anamtumia Pasta Nkuku pesa kupitia mtandao wa M-Pesa na kwamba hawakuandikiana mkataba wowote.

Bi Teeti alimweleza hakimu kwamba ana rafiki ambaye atafika kortini kutoa ushahidi. Alisema ndiye alikuwa shahidi wake.

Taarifa za M-Pesa na benki zilizowasilishwa kortini zilionyesha kwamba kati ya Desemba 8 na Desemba 10, 2020, Bi Teeti alikuwa amempa Bw Nkuku Sh1,020,000.

Pesa hizo zilikuwa pamoja na zile alizokuwa ametoa kutoka Benki ya Co-operative.

Pesa hizo kutoka kwa Benki zilikabidhiwa Pasta na rafikiye mlalamishi.

“Nilimuamini Bw Nkuku sana kiasi ya kwamba sikuona haja ya kuweka mkataba ama kutembelea boma lake kuona mifugo aliyokuwa amenunua,” alisema mlalamishi akitoa ushahidi mbele ya Bw Ondieki.

Muumini huyo alisema alimwamini Bw Nkuku hata akampa gari lake aina ya Pick-up baada ya pasta kumweleza Mungu alikuwa amemzugumzia kwamba amkabidhi gari hilo aliombee na kulitakasa.

“Pasta alikaa na gari langu hadi pale maafisa wa uchunguzi wa jinai walipoingilia kulinusuru,” alisema.

Mahakama ilifahamishwa kwamba mlalamishi aliendelea kutuma pesa za kununua mifugo hadi zikafika Sh2,664,109.

Alimweleza mchungaji wake kwamba angeenda kuona mifugo aliyonunua lakini pasta akaanza ujanja wa kusema hakuwa nyumbani.

Mahakama iliambiwa Bw Nkuku alianza tabia ya kusema hayuko nyumbani na hatimaye akazima simu yake.

“Niligutuka na kujua kabisa mambo yalienda mrama baada ya pasta kukataa nikimtembelea kuona ng’ombe wangu. Ni wakati huo niliwaeleza maafisa wa DCI kisha wakachunguza,” alisema.

Bw Nkuku alikamatwa na kushtakiwa baada ya kutambulikana hakuna mifugo aliyonunua ila alimlaghai muumini wake.

Mshtakiwa amekana kwamba alimlaghai mlalamishi Sh2,664,109 kati ya Machi 1, 2021, na Aprili 30, 2023, akidai atamnunulia ng’ombe wa kufuga.

Pesa hizo alikabidhiwa Bw Nkuku jijini Nairobi.

Shtaka lilisema mshtakiwa alijua anadanganya hakuwa ananunua ng’ombe.

Ni wakati huo Bi Teeti alimtazama Bw Nkuku na kuomba mahakama impiganie apate tena pesa zake alizopoteza katika kashfa hiyo.

“Naomba hii mahakama initetee angalau nirudishiwe pesa zangu. Naomba nipate haki hapa kortini,” Bi Teeti alimsihi hakimu.

Kesi hiyo iliahirishwa hadi Aprili 15, 2024, ushahidi utakapowasilishwa na Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP).