Dondoo

Pasta atimua mke kwa kuenda kwao bila idhini

March 21st, 2018 1 min read

Na JOHN MUSYOKI

KIAMBERE MJINI

PASTA mmoja mjini hapa alishangaza majirani kwa kumfukuza mkewe alipoenda kutembelea jamaa zake mashambani bila idhini yake.

Inasemekana pasta alipoondoka kuenda kuhubiri, mkewe alifunga safari kuenda kutembelea jamaa zake bila kumfahamisha.

Duru zinasema pasta aliporejea nyumbani baada ya kushinda siku nzima akihubiri, alishangaa kupata mlango wa nyumba ukiwa umefungwa kwa kufuli.

Alimpigia mkewe simu lakini ilikuwa mteja. Kwa hasira pasta alianza kufoka na kushangaza majirani.

“Nilioa mwanamke wa sampuli gani mimi. Yaani mke wangu alifunga nyumba na kuondoka bila kuniarifu na simu yake ni mteja. Usiku umeanza kuingia na nimechoka sana ninataka kupumzika,” pasta alifoka.

Baada ya saa mmoja mke wa pasta alirejea na kupata mumewe ameketi nje ya nyumba kwenye kiti alichoomba kwa jirani. Inasemekana alianza kumfokea mkewe papo hapo akimlaumu kwa kuenda kutembea bila kumfahamisha.

“Umetoka wapi? Yaani uliamua kunitesa. Nataka unieleze umetoka wapi. Ulifunga nyumba na ukaondoka na funguo na nilipokupigia simu ilikuwa mteja,” pasta alikuja juu.

Kulingana na mdokezi, mkewe alimweleza ukweli wa mambo.

“Nimetoka nyumbani kutembelea jamaa zangu. Umekuwa ukinipuuza nikikuambia ninataka kuenda kusalimia jamaa zangu,” mke wa pasta alisema. Penyenye zasema pasta alitishia kumfurusha mkewe kwa kumkaidi.

“Nipe funguo za nyumba yangu na urudi huko kwenu na ukitosheka kusalimia jamaa zako utarejea,” pasta alisema.

Ilibidi mke wa pasta kutulia kwa jirani yake kwa sababu giza lilikuwa limeingia na pasta hakumruhusu kuingia ndani ya nyumba. Hata hivyo, baada ya hasira kutulia alimwita nyumbani na kumuonya asiwe akienda mbali bila kumfahamisha.

…WAZO BONZO…