Habari Mseto

Pasta azirai na kufa katika mzozo wa chai na binti yake

January 21st, 2019 2 min read

BENSON AMADALA na MACHARIA MWANGI

UGOMVI kati ya pasta mstaafu wa Kanisa la Church of God eneo la Ingotse, Kaunti ya Kakamega na bintiye kuhusu chai ulipelekea kifo cha mzee huyo mnamo Ijumaa.

Habari zilielea kuwa Pasta Gabriel Amayo Nangabo,76, kutoka kijiji cha Ematetie, Kata ya Butsotso ya Kati, alikasirishwa na hatua ya mwanawe wa miaka 21 kumwaga chai ambayo mkewe alikuwa ametayarisha.

Kulingana na mkewe Pasta Amayo, Bi Beatrice Amanya, alikuwa jikoni akimpikia mumewe chai ndipo mwanawe akaingia akiwa amepandwa na hasira na kuzua ugomvi.

“Mwanangu alichukua birika iliyojaa chai akaimwaga. Babake alipoingilia kati aliendeleza ukatili kwa kuanza kutupiga kwa mawe,” akasema Bi Amanya kwa masikitiko.

Kulingana na jirani Alfred Kitayi, alivutiwa na kelele na vishindo hivyo na alipofika alpiata mzee huyo ameanguka chini akiwa ameaga dunia.

Bi Amanya alifichua kwamba mwanawe amekuwa msumbufu tangu awache masomo baada ya kupata mimba.

OCPD wa Kakamega John Chebii alithibitisha kisa hicho na kusema kwamba msichana huyo amekamatwa na polisi wanaendelea uchunguzi.

“Tunasubiri matokeo ya uchunguzi wa maiti kabla ya kuamua iwapo tutamshataki msichana huyo,” akasema Bw Chebii.

Katika Kaunti ya Nakuru, afisa polisi wa Utawala (AP) alimpiga risasi na kumjeruhi mhudumu wa duka la M-Pesa mwenye umri wa miaka 18, kabla ya kujitoa uhai kwa risasi katika eneo la Ndabibi.

Mkuu wa polisi wa eneo hilo, Bw Samuel Waweru aliambia wanahabari kwamba afisa huyo alienda katika duka hilo Jumamosi asubuhi na akampiga risasi mhudumu huyo.

Bw Waweru alieleza kuwa msichana huyo alipata majeraha na akakimbizwa katika Hospitali ya Kaunti Ndogo ya Naivasha ambako anaendelea kupokea matibabu.

“Nimewasiliana na msimamizi wa hospitali na amesema tineja huyo anaendelea vyema,” akasema Bw Waweru.

Mkuu huyo wa polisi, ambaye alikuwa akizungumza katika eneo la tukio, alisema baada ya kumfyatulia msichana huyo risasi, afisa huyo alienda nyumbani kwake ambapo alijipiga risasi na kujiua.

Mwili wake ulipelekwa katika hifadhi ya maiti ya Hospitali ya Kaunti Ndogo ya Naivasha.