Habari za Kaunti

Pasta mashakani kwa kuhangaisha wafuasi wake kingono

January 29th, 2024 2 min read

NA WYCLIFFE NYABERI

POLISI mjini Kisii wanamsaka mchungaji wa kanisa la Pentecostal Assemblies of God (PAG), anayedaiwa kunajisi mwanafunzi wa darasa la nne wa miaka 10 katika eneo la Kiogoro eneobunge la Nyaribari Chache mnamo Jumamosi Januari 27, 2024.

Mtoto huyo anasemekana kutumwa na mamake ampelekee pasta kiamsha kinywa alichokuwa amemwandalia lakini inadaiwa “mtumishi huyo wa Mungu” anayeishi kanisani alimgeukia na kumdhulumu kingono.

“Iliripotiwa na Kwamboka (si jina lake halisi), mkazi wa kijiji cha Riang’ombenene, Lokesheni ya Amariba kwamba alimtuma msichana wake ampelekee pasta Duke Morang’a wa Nyabonda PAG, kiamsha kinywa alichokuwa amemwandalia majira ya saa 7.30 asubuhi. Alipowasili kanisani, mchungaji huyo alimwelekeza hadi kwenye makazi yake yaliyoko ndani ya kanisa hilo ambako inadaiwa alimvua nguo kabla ya kumnajisi,” sehemu ya ripoti ya polisi iliyoonwa na Taifa Leo Dijitali ilisema.

Baada ya kitendo hicho mchungaji huyo anadaiwa kumpangusa mtoto huyo mapaja kwa taulo na kisha kumpa sarafu ya Sh5 kabla ya kumwacha.

Alipofika nyumbani, alimweleza mama yake masaibu aliyopitia.

Mama huyo aliripoti katika kituo cha polisi cha Kiogoro na kulazimu maafisa kufuatilia kisa hicho.

Kwa upesi, walielekea nyumbani kwa pasta lakini hawakumpata kwani alikuwa amekimbilia kusikojulikana.

“Bado tunamtafuta mshukiwa na haitachukua muda mrefu kabla ya kumtoa katika maficho yake,” kamanda wa polisi wa Kaunti ya Kisii Charles Kases aliambia Taifa Leo Dijitali kwa njia ya simu.

Mwathiriwa alipelekwa katika Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Kisii (KTRH) kufanyiwa vipimo.

Polisi walipata taulo iliyodaiwa kutumika kupangusa mapaja ya mwanafunzi huyo na chai ya mkandaa ambayo ilikuwa kwenye kijikontena cha lita moja.

Kisa hicho kinajiri wiki moja tu baada ya kisa kingine cha unajisi kuripotiwa katika eneo la Magena, eneobunge la Bomachoge Borabu.

Mark Okemwa Manono, 30, alifikishwa mahakamani wiki jana baada ya kudaiwa kunajisi msichana wa miaka mitano mnamo Januari 20, 2024 katika kituo cha biashara cha Magena.

Tukio hilo liliibua hisia kutoka kwa mke wa Naibu Rais Rigathi Gachagua, Bi Dorcas Rigathi aliyekuwa ziarani Kisii wakati huo.

Pamoja na gavana wa Kisii Simba Arati, walizitaka asasi zinazohusika kushughulikia suala hilo zifanye hima.

[email protected]