Pasta mfuska anusurika kichapo

Pasta mfuska anusurika kichapo

Na JOHN MUTUKU SAMUEL

KIBINGOTI, Kirinyaga

PASTA wa kanisa moja eneo hili hakuamini arubaini zake zilipofika akajipata akinyenyekea mshirika wake asimdhuru kwa kumnyemelea mkewe.

“Naweza kukumegamega vipande vipande usitambuliwe hata na mkeo,” polo alimtishia pasta, akimkabidhi zawadi ya makofi mawili mazito.

“Ndugu yangu, usilipize kisasi. Naomba unionee huruma sitarudia tena. Haya ni majaribu ya kishetani,” pasta alizidi kunyenyekea kwa majonzi.

Pasta, buda aliye stadi wa kueneza injili alikuwa ameanza tabia ya kutembea na mke wa polo.

Mapasta marafiki zake walimuonya lakini akawa hasikii la mwadhini wala la mtekamaji msikitini.

“Mke wa mtu ni sumu. Huyu haogopi kifo?” pasta mmoja aliuliza.

“Sikio la kufa halisikii dawa. Mwacheni ale asali itakapomgeuka atajua Mungu keshamuacha,” pasta mwingine alichangia.

Siku ya siku, pasta aliegesha gari lake nyumbani kwa polo saa kumi alfajiri.

Jirani aliyejua kilichoendelea alimpigia polo simu na kumtaka afike kwake upesi.

Polo anafanya kazi ya ubawabu nyumbani kwa matajiri, karibu na kwake.

Polo alipoambiwa ‘mgeni’ wa usiku alikuwa nyumbani kwake alifika mbio mbio na kumfumania pasta kitandani kwake akiendelea kuuchovya mzinga.

Polo alivua koti la heshima, akamtandika pasta kwa mjeledi ambao ulimbambua mgongo vibaya vibaya.

“Mshirika wangu, utaniua jamani. Haya ni mambo tunayoweza kuzungumza,” pasta aliomba.

“Sitaki kuyazungumza na wewe. Mbwa kasoro mkia,” polo alisema akimvaa pasta tena na kumwangushia mvua ya makonde na mateke.

Kama si majirani, ‘Mtumishi wa Mungu’ angekiona cha mtema kuni.

Zimepita wiki mbili tangu mkasa huo na inasemekana pasta amesameheana na polo naye amekoma tabia ya kufukuzana na wake za watu.

You can share this post!

Polisi wasaka mshukiwa wa ugaidi aliyekwepa mtego wao

KAMAU: Viongozi sasa waelekeze macho kwa umoja wa taifa