Dondoo

Pasta mgeni atoroka na kapu la sadaka waumini wakiomba

February 19th, 2019 1 min read

NA CORNELIUS MUTISYA

MISUUNI, KATHIANI

Hali ya mshikemshike ilizuka eneo hili pasta mgeni alipotoroka na kikapu kilichojaa sadaka waumini walipokuwa wamezama katika maombi.

Kulingana na mpambe wetu, pasta wa kanisa hilo alimualika mwenzake kutoka kaunti jirani ili awalishe waumini chakula cha kiroho na baadaye kuongoza harambee ya kupanua kanisa hilo.

“Mtumishi wa Mungu alikuwa na matumaini makubwa kuwa mwenzake angechangisha pesa nyingi katika harambee hiyo kwa sababu alikuwa na ufasaha wa kuongea. Hii ndio sababu kuu ya kumualika kanisani,” alisema mdokezi.

Twaarifiwa kwamba, wakati wa ibada ulipowadia, kanisa lilikuwa limejaa pomoni. Wanakwaya walianza kwa kughani nyimbo mbili na baadaye pasta akanyanyuka ili amualike mgeni wake awalishe waumini chakula cha kiroho.

“Mahubiri ya pasta huyo mgeni yalikuwa moto moto na yaliwagusa wengi rohoni,” asema mdaku wetu.

Inasemekana kwamba, sadaka zilitolewa kwa wingi na kikapu kikawekwa madhabahuni alipokuwa ameketi pasta huyo mgeni.

Inadaiwa kwamba pasta wa kanisa hilo aliinuka na akawaongoza waumini kwa maombi kabla ya kuanza mchango.

Kila mmoja alianza kuomba kwa ndimi na kupandwa na jazba! Ni wakati huo pasta mgeni alipochukua kikapu kilichojaa sadaka na akaondoka polepole na kutoroka kupitia kichaka kilichoko karibu na kanisa.

Penyenye za mtaa zaarifu kuwa, waumini walipomaliza maombi, walipigwa na butwaa walipopata mgeni alikuwa ametoroka na sadaka yote.

Hata hivyo, jitihada zao za kumsaka ziliambulia patupu maana alikuwa ametokomea kusikojulika na akafunga simu yake.

Waumini na pasta wao walibaki wameduwaa kutokana na kisa hicho cha kustaajabisha huku wakimlaani kwa kuiba sadaka bila kuhofia kipigo kutoka kwa Mungu. Pasta wao aliapa kumsaka mgeni wake ili achukuliwe hatua za kisheria.