Dondoo

Pasta mla fuska abanwa na kidosho

June 30th, 2019 1 min read

Na Leah Makena

ISINYA, KAJIANDO

Pasta wa hapa, alilazimika kumkabidhi kidosho mmoja sadaka iliyotolewa kanisani ili asianike vitendo vyake vya kula fuska.

Kulingana na mdaku wetu, kipusa alikuwa mpango wa kando wa pasta. Alikuwa akimtembelea mwanadada huyo usiku kula uroda na kisha kurejea kwake kwa sababu alikuwa na familia.

Baada ya miezi kadhaa, pasta alichoshwa na huduma za kipusa huyo na akaamua kumtema lakini akashindwa kwani mrembo alidai alikuwa amemzoea.

Juhudi za pasta za kumshawishi kidosho waachane kwa sababu alikuwa ameoa na ni mchungaji, ziliambulia patupu kwani kidosho alianza kudai pesa kutoka kwake tena kwa vitisho.

Mwanadada alimtaka pasta amwajiri kazi katika kanisa alilokuwa akihudumu lakini akakataa akihofia uhusiano wao ungenduliwa.

Hapo ndipo kidosho alianza kudai hela za kujikimu huku mbinu zote za pasta za kumhepa zikigonga mwamba.

Hivi majuzi, pasta alikatiza mazungumzo na mwanadada. Hata hivyo, alishangazwa kuona mrembo kwenye kanisa lake.

Siku hiyo, kidosho aliomba shemazi kumpeleka hadi ofisi ya pasta akisema alikuwa mgeni wake.

Pasta hakuamini macho yake kidosho apojitoma ndani ya ofisi na kuanza kumfokea kama mtoto mdogo.

“Mbio zako za sakafuni zimeishia ukingoni kwani leo nimekupata. Unawezaje kunihepa ukijua wazi kuwa sina ajira? Mbona hauna utu na nilikuwa nikikuburudisha? Nataka kodi ya nyumba na pesa ya shopping,” kidosho aliwika.

Kwa kuhofia kuanikwa mbele ya washiriki waliokuwa wakimsubiri, pasta alilazimika kumkabidhi sadaka iliyokuwa imetolewa siku hiyo na mwanadada akaondoka akitabasamu.

Pasta alibaki kukadiria hasara asijue la kufanya kwani hakuwa na uwezo wa kuhama kanisa hilo.