Dondoo

Pasta mpenda pesa abaki bila waumini

October 17th, 2019 1 min read

Na SAMUEL BAYA

LANGAS, NAKURU

PASTA wa kanisa moja la mtaani alibaki pweke kanisani baada ya waumini kumtoroka wakidai ni mkora.

Kilichowakera zaidi waumini ni tabia ya pasta huyo pamoja na mkewe kuwalazimisha watoe kiwango fulani cha pesa kila Jumapili.

Kulingana na mdokezi wetu, pasta amekuwa na mazoea ya kuwapa waumini kipimo cha sadaka wanayofaa kutoa; kuanzia Sh200 hadi Sh500, bila kujaji mapato yao.

“Watu hawaendi tena katika kanisa hilo kwa sababu pasta na mkewe wamekuwa madikteta. Ukitoa pesa kidogo, kama Sh50, wanakuchekelea mbele ya watu. Tumeshindwa kama huyu ni mtumishi wa Mungu kweli ama ni mlaghai,” alisema mmoja wa waliokuwa waumini katika kanisa hilo.

Inasemekana pasta huyo aliamua kuwarai wazee wa kanisa waende kushawishi watu mtaani wajiunge na kanisa lake.

“Juzi alimfuata mzee mmoja wa kanisa akitaka awatafute waumini, lakini hiyo ni vigumu kwani watu mtaani wanamjua mchungaji huyo kuwa mpenda pesa,” alisema mwumini huyo.

Inadaiwa kwamba mtumishi huyo wa Mungu aligundua hali sio shwari, baada ya watu ambao walianzisha naye kanisa hilo kuamua kuondoka waliposhindwa kuhimili vituko vyake.

“Kuna watu ambao walianza pamoja kanisa hilo lakini baada ya kuona tabia yake ya kushangaza, waliamua kuondoka. Sasa ni kana kwamba kila kitu kimemshinda. Hakuna tena dalili za watu kurudi katika kanisa hilo,” akasema mdokezi wetu.

Kwa sasa duru zilituarifu kuwa pasta amebadili mbinu na sasa ameanza mikakati ya chini kwa chini jinsi atakavyorejesha waumini hao. Hii ikiwa ni pamoja na kuwatembelea binafsi katika nyumba zao akiomba warudi kanisani.